LIBYA-MAREKANI-UINGEREZA

Waasi wazidi kukaribia Mji wa Bani Walid anakotajwa kujificha Kanali Muammar Gaddafi

Wapiganaji wa Baraza la Mpito la Waasi Nchini Libya NTC wamezidi kusonga mbele na sasa wamebakiza Mji mmoja tu wa mwisho ambao unahisiwa ndipo Kiongozi wa nchi hiyo anayetakiwa kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi amejificha.

Matangazo ya kibiashara

Mji ambao unadhani ndipo mahali alipo Kanali Gaddafi kwa sasa ni Bani Walid ambapo wapiganaji wa waasi wamesema wameuzunguka kwa kiasi kikubwa na wakati wowote huenda wakamkamata Kiongozi huyo.

Mohamed Al Fassi ambaye ni Kamanda katika vituo vya ukaguzi kwenye Kijiji cha Shishan kilichopo kilometa 70 Kaskazini mwa Mji wa Bani Walid amenukuliwa akisema wapo mbioni kumtia nguvuni kanali Gaddafi pamoja na askari wake watiifu.

Kamanda Al Fassi amesema mazungumzo baina yao na askari wa watiifu wa Kanali Gaddafi ambao waliahidi kumsalimisha Kiongozi huyo yamefikia tamati kutokana na wenzao kutokuwa na utayari wa kufanikisha jambo hilo.

Waziri Mpya wa Mambo ya Ndani wa Libya kupitia Baraza la Mpito la Waasi NTC Ahmed Darrat ameweka bayana kuwa Mji wa Bani Walid utakuwa huru kwenye mikono yao leo ama kesho kutegemea na upinzani ambao watakutana nao.

Kwa upande wake Msemaji wa NTC katika eneo hilo Mahmud Abdelaziz amesema wanasubiri amri kutoka kwa wakuu wao ili waweze kuvamia Mji wa Bani Walid na kuweza kumaliza kazi ya kuweka maeneo yote ya nchi hiyo chini ya himaya yao.

Abdelaziz amesema hapo jana askari watiifu kwa Kanali Gaddafi walitaka kukimbia lakini walikumbana na wapiganaji wao kitu ambacho kichangia kutokea kwa mapigano yaliyodumu kwa dakika kadhaa.

Msako dhidi ya kanali Gaddafi na askari wake watiifu unaendelea wakati ambapo tayari Mwenyekiti wa NTC Mustafa Abdel Jalil akitangaza muda zaidi kwao kujisalimisha kabla ya wao kuchukua hatua zaidi.

Katika hatua nyingine nyaraka za siri ambazo zimepatikana nchini Libya zinaonesha ushirkiano uliopo baina ya Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, Shirika la Kijasusi la Uingereza MI6 pamoja na Utawala wa Kanali Gaddafi.

Tayari Uingereza kupitia kwa Waziri wake wa Ulinzi William Hague amekanusha ukweli wa nyaraka hizo na kuweka kuwa ushirikiano ulikuwa zamani na siyo katika kipindi hiki ambacho wao wamehusika kuwasaidia Waasi.

Mapigano nchini Libya yamedumu kwa zaidi ya miezi sita na kushuhudia Waasi wakifanikiwa kuuangusha uatawala wa Kanali Gaddafi katika sehemu kubwa ya nchi hiyo wakisaidia na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.