BANI WALID-LIBYA

Wapiganaji wa waasi katika miji ya Sirte na Bani Walid warudisha vikosi vyuma kufuatia upinzani mkali toka kwa wanajeshi wa Gaddafi

Wapiganaji wa waasi wakiwa katika njia ya kuelekea mji wa Bani Walid
Wapiganaji wa waasi wakiwa katika njia ya kuelekea mji wa Bani Walid Reuters

Wapiganaji wa waasi nchini Libya walioko mstari wa mbele kuingia katika mji wa Bani Walidi wamelazimika kukimbia eneo hilo kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na wanajeshi wa kanali Muamar Gaddafi waliokataa kujisalimisha.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa wapiganaji hao amesema kuwa wamelazimika kuondoka katika mji huo kufuatia upinzani mkali walioupata toka kwa wapiganaji wa kanali Gadafi ambao wanatumia silaha nzito zaidi pamoja na bunduki maalumu za shabaha.

Mapigano hayo ambayo yalidumu kwa siku nzima ya Ijumaa ndivyo yalivyokuwa pia katika mji wa Sirte ambako nako wapiganaji hao wameondoa vikosi vyao baada ya kuripotiwa vifo vya wapiganaji kumi na moja wa waasi.

Msemaji wa kanali Gaddafi Moussa Ibrahim ambaye nae yuko mafichoni kama kiongozi wake, alinukuliwa mara baada ya waasi hao kuondoka katika miji hiyo akisema kuwa wanajeshi wake wanaendelea kukusanya silaha zaidi na kujiandaa na vita vya muda mrefu zaidi.

Akiongea na kituo kimoja cha televisheni nchini Syria, msemaji huyo ameongeza kuwa vita hivyo bado sana kusema kwamba vimemalizika kama waasi wanavyodai, badala yake vikosi vyake vitajibu mashambulizi ya aina yoyote na kwa nguvu yatakayofanywa na waasi.

Msemaji huyo pia amevishutumu vikosi vya majeshi ya NATO akisema kuwa anashangazwa na ndege zake ambazo zimekuwa zikishambulia makazi ya watu na Hospitali katika miji ya Sirte na Bani Walidi hali aliyosema wananchi wakawaida ndio wanaoumia.

Baraza la mpito nchini humo juma hili lilitangaza mazungumzo kushindikana katika miji hiyo na kwamba vikosi vyake vimeanza mashambulizi katika ngome hizo kwa lengo la kuvisambaratisha vikosi vya Gaddafi opereseheni inayoonekana itachukua muda kukamilika.