PALESTINA-MAREKANI

Furaha yatanda nchini Palestina huku maswali yakitanda iwapo ombi lao litakubaliwa

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akiwa na mfano wa barua aliyoiwasilisha Umoja wa Mataifa UN kuomba uanachama
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas akiwa na mfano wa barua aliyoiwasilisha Umoja wa Mataifa UN kuomba uanachama Reuters/M.Segar

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ametekeleza jambo la kihistoria kwa taifa lake baada ya kufanikiwa kuwasilisha rasmi ombi la nchi hiyo kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa UN huku hatua yao ikionekana kuungwa mkono na wanachama wengi ukiondoa Marekani ambayo imetangaza kupinga hilo.

Matangazo ya kibiashara

Rais Abbas mbele ya wajumbe ambao wanahudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa UN nchini Marekani ameweka bayana wakati umefika kwa nchi hiyo kutambuliwa rasmi kama taifa huru na Umoja huo.

Palestina inasaka kwa udi na uvumba uanachama wa Umoja wa Mataifa UN na iwapo itafanikiwa inatarajiwa kuwa nchi mwanachama wa mia moja na tisini na nne kwani hadi sasa kuna wanachama mia moja na tisini na tatu pekee.

Baada ya kuwasilishwa rasmi kwa ombi hilo kwenye Jukwaa la Hotuba la Umoja wa Mataifa UN mamia ya wajumbe walionekana kuridhia ombi hilo lakini wawakilishi kutoka Marekani walionekana wakiendelea na shughuli zao kana kwamba hakukuwa na chochote kinachoendelea.

Nchini Palestina kwenyewe maelfu ya wananchi walijitokeza katika Miji ya Ramallah pamoja na Ukingo wa Gaza kusikiliza hotuba hiyo ya kihistoria kutoka kwa Rais Abbas ambapo wengi walikuwa wakisema Mwenyezimungu Mkubwa na Mioyo yetu na Damu zetu tutapambana kuitetea Palestina.

Wananchi hao walionekana kuwa na furaha isiyo na kifani baada ya ombi lao kuonekana kuungwa mkono na kisha kupokelewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon kwa ajili ya kushughulikiwa.

Licha ya wananchi hao kujitokeza mitaani na kuendelea kuimba nyimbo sambamba wakiwa na bendera za Palestina lakini kumeendelea kuwa na maswali mengi magumu iwapo ombi hilo litafanikiwa kwani tayari Marekani imejinadi kutumia kura yake ya turufu kuzima ndoto hizo za Palestina.

Katika Mji wa Ukanda wa Gaza ambapo ni Ngome imara ya Chama Cha Hamas hali ilikuwa tofauti kwani wananchi walikatazwa hata kuangalia hotuba hiyo huku wengine wakiondolewa kwenye maeneo ya wazi walipokuwa wanaonesha uwasilishaji wa ombi hilo.