URUSI

Vladimir Putin kuwania Urais nchini Urusi mwaka 2012 baada ya kupendekezwa na Rais Dmitry Medvedev

Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin apendekezwa kuwania Urais mwaka 2012
Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin apendekezwa kuwania Urais mwaka 2012 REUTERS/Yana Lapikova

Rais wa Urusi Dmitry Medvedev ametangaza rasmi kumpendekeza Waziri Mkuu Vladimir Putin kuwa mgombea wa nafasi ya urais kupitia Chama Tawala nchini humo kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka elfu mbili kumi na mbili na iwapo atafanikiwa ataongoza kwa kipindi cha miaka sita.

Matangazo ya kibiashara

Rais Medvedev ametangaza uamuzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Tawala na kuweka bayana baada ya uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi yeye atachukua nafasi ya kuwa Waziri Mkuu chini ya utawala mpya wa Rais Putin.

Mamia ya wajumbe ambao wamehudhuria mkutano huo walionekana kushangilia baada ya kutangazwa kwa uamuzi wa Putini kuwa mgombea wa urais kupitia Chama Tawala kwenye kinyang'anyiro kijacho cha uchaguzi nchini Urusi.

Medvedev amesema itakuwa ni busara kubwa kwa wajumbe wengine wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho kuunga mkono pendekezo hilo la Mwenyekiti wao kuwania urais kwa ngwe nyingine.

Kiongozi huyo wa Urusi ameweka bayana uchaguzi mkuu ukimalizika na Putin akiwa mshindi ataendelea kufanya naye kazi kwa ushirikiano katika kuhakikisha taifa hilo linakuwa na mabadiliko makubwa zaidi ya ilivyo sasa.

Tayari Waziri Mkuu Putin ametangaza hiyo ni heshima kubwa kwake kukiwakilisha Chama chake kwenye uchaguzi mkuu ujao na kuwashukuru wale wote ambao wameunga mkono pendekezo hilo.

Waziri Mkuu Putin amesema atahakikisha anaendelea kushirikiana na wanachama wote wa chama hicho katika kuhakikisha wanashinda kwenye kinyang'anyiro hicho cha mwake elfu mbili kumi na mbili na kuwaletea maendeleo wananchi.

Mshindi wa Uchaguzi wa rais nchini Urusi atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka sita badala ya ilivyokuwa awali ambapo waliongoza kwa kipindi cha miaka minne baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya katiba yaliyoongozwa na Rais Medvedev.

Waziri Mkuu Putini aliondoka madarakani kwenye Ikulu ya Kremlin baada ya uchaguzi Mkuu mwaka elfu mbili na nane na hivyo kuchukua wadhifa wake mpya ambao anaushikilia hadi sasa chini ya Rais Medvedev.