LIBYA

Wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito NTC waendelea kulisogelea Jiji la Sirte

Wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito NTC wakiwa Magharibi mwa Jiji la Sirte
Wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito NTC wakiwa Magharibi mwa Jiji la Sirte (Reuters)

Wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito nchini Libya NTC wameendelea kusonga mbele katika Mji aliozaliwa Kanali Muammar Gaddafi wakiwa katika harakati zao za mwisho za kutaka kuiweka miji yote chini ya himaya yao baada ya eneo kubwa la nchi hiyo kuwa chini ya ulinzi wa wapiganaji hao.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji hao wapo Mashariki mwa Jiji la Sirte ambalo wanaamini ifikapo kesho watakuwa wameliweka katika himaya yao kwani siku ambazo wametoa kwa askari watiifu kwa Kanali Gaddafi kujisalimisha zinafikia tamati leo jumamosi.

Mamia ya wananchi yamekimbia katika Jiji la Sirte huku mmoja wa Makamanda wa NTC akisema askari watiifu wa Kanali Gaddafi wamekuwa wakifanya mashambulizi yao kulenga raia wa nchi hiyo ambao wanaamini hawana makosa yoyote.

Wapiganaji wa NTC wamekiri kuendelea kukumbana na upinzani na mashambulizi kutoka kwa askari watiifu wa Kanali Gaddafi wakati huu ambapo wanajiandaa kulichukua Jiji la Sirte ambalo linaonekana ni miongoni mwa ngome kongwe kwa Kiongozi huyo ambaye amefurushwa madarakani.

Mji mwingien ambao bado wapiganaji hao wanahaha kuuweka kwenye himaya yao ni Bani Walid ambapo kuna askari wengi watiifu kwa Kanali Gaddafi ambao wamekuwa wakiwapa wakati mgumu.

Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO yamesema yapo katika hatua ya mwisho kuhakikisha Jiji la Sirte linakuwa kwenye himaya ya Baraza la Taifa la Mpito NTC huku Kamanda wa Baraza hilo Ahmed Zlitni akinukuliwa wamedhibiti mlango wa kuingilia Jiji hilo.

Katika hatua nyingine Mtoto wa kike wa Kanali Muammar Gaddafi, Aisha amesema baba yake yupo salama kabisa na anaendelea na mapambano makali huku akiwashambulia kwa maneno watawala wapya na kuwaita ni wasaliti wakubwa.

Aisha, kaka zake wawili pamoja na mama yao Safiya ambao walikimbilia nchini Algeria wameendelea kusema Viongozi wa NTC ni wasaliti wakubwa ambao wamekiuka ahadi ambazo walikuwa wamezitoa.

Huu ni mwezi mmoja sasa tangu Waasi wavamie makazi ya Kanali Muammar Gaddafi yaliyopo Tripoli na kumfanya akimbilie kusikojulikana huku taarifa zikimhusisha kuwepo Bani Walidi huku wengine wakisema amekimbilia katika nchi jirani ikiwemo Burkina Faso.

Tangu kuanza kwa machafuko nchini Libya yamedumu kwa miezi saba sasa huku Waasi wakifanikiwa kuweka utawala mikononi mwao baada ya kusaidia kwa kiasi kikubwa na mashambulizi ya Majeshi ya NATO.