Libya

Msemaji wa NATO: Mashambulizi ya NATO yamdhoofisha Gaddafi katika miji ya Sirte na Bani Walid

Reuters/Goran Tomasevic

Wapiganaji wa Baraza la Taifa la Mpito nchini Libya NTC wamejinadi kuweka kwenye himaya yao Bandari iliyopo katika Jiji la Sirte eneo ambalo Kanali Muammar Gaddafi amezaliwa na ana wafuasi wengi kwa sasa.

Matangazo ya kibiashara

Wasemaji wa NTC wamesema wamefanikiwa kuchukua umiliki wa bandari hiyo pasina kukabiliwa na upinzani mkali lakini wameendelea kukutana na wakati mgumu katika Mji wa Ban Walid ngome nyingine ya Kanali Gaddafi.

Msemaji wa Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO Roland Lavoie akiwa Naples, Italy amesema Kanali Gaddafi kwa sasa hana chake tena katika nchi hiyo kwani mashambulizi ambayo yamefanyika yamemdhoofisha.

NATO imesema wapiganaji wanaomtii Kanali Muammar Gaddafi wanajificha katika maeneo ya raia, na kuwaweka watu hao katika hatari kubwa.

Msemaji wa NATO kanali Roland Lavoie amesema katika miji hiyo ambayo bado iko chini ya wapiganaji wanaomtii Gaddafi, inakabiliwa na uhaba wa maji ya kunywa, chakula na dawa.

Wapiganaji kutoka Baraza la Mpito la Taifa la Libya wamezidi kushambulia miji hiyo miwili. Hayo ni maeneo makuu mawili ya mwisho ambayo bado yako chini ya udhibiti wa wafuasi wa Gaddafi.

Baraza la Mpito la Taifa, NTC, linasema ni suala tu la wakati kabla ya miji hiyo kutwaaliwa na majeshi yake.