LIBYA

Mapambano makali yaendelea kati ya Wapiganaji wa NTC na Askari wa Kanali Gaddafi

Reuters/Goran Tomasevic

Wapiganaji wa Serikali ya Baraza la Mpito la Taifa nchini Libya NTC wameendelea kukabiliana vilivyo na askari watiifu wa Kanali Mummar Gaddafi katika Mji aliozaliwa wa Sirte.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji wa NTC wamesema kuwa wanasonga mbele kwa kasi na tayari yamefanikiwa kuweka kwenye himaya yao karibu asilimia zaidi ya hamsini ya Mji huo wa Sirte ambao ulikuwa chini ya askari watiifu kwa Kanali Gaddafi.

Mapambano hayo ambayo yanatajwa kudumu kwa muda wa mwezi mzima kwa lengo la kuuteka Mji wa Sirte yameonekana dhahiri ni magumu kwa pande zote licha ya taarifa kutoka NTC kusema wamefanikiwa kusonga mbele.

Makabiliano hayo yamechangia watu wengine kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kitu ambacho kimewafanya wengi kukosa huduma za matibabu kutokana na madaktari kukimbia mapigano hayo.

Huduma muhimu kama madawa na maji zimeendelea kuhitajika lakini zimekosekana wakati huu ambapo askari watiifu kwa Kanali Gaddafi wakiendelea kutetea miji michache ambayo wanaishikilia.

Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu Dibeh Fakhr amesema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa vitanda na madawa katika Jiji la Sirte kutokana na kuzidiwa na idadi kubwa ya majeruhi.

Kiongozi wa Kamandi ya Kijeshi ya NTC Salem Gheith naye amenukuliwa akisema wamepoteza wapiganaji wao kwenye mapigano abayo yalianza tangu siku ya jumapili baina yao na askari watiifu kwa Kanali Gaddafi.

Katika hatua nyingine wapiganaji wa NTC kumi na saba wamepoteza maisha huko Bani Walid katika mashambulizi mengine ya kutaka kuuchukua mji huo ambao nao unashikiliwa na askari watiifu kwa Kanali Gaddafi.

Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO kupitia Katibu Mkuu wake Andres Fogh Rasmussen ameendelea kusifia operesheni ambayo waliifanya nchini Libya na kusema inakaribia mwishoni.

Takwimu zinaonesha kuwa NTC hadi sasa imepoteza zaidi ya wapiganaji sabini katika mapambano ambayo yanaendelea katika Mji ya Sirte na Ban Walid ambapo wakazi wake wanatajwa kukimbia.