NEW ZEALAND

Serikali ya New Zealand imesema kuvuja kwa mafuta baharini ni janga la taifa

Serikali ya New Zealand imesema kuwa kuvuja kwa mafuta kutoka kwenye meli ya MV Rena ambayo imekwama katika pwani ya kisiwa cha Plenty kaskazini mwa nchi hiyo ni janga kubwa la kimazingira kuwahi kutokea katika taifa hilo

SUN MEDIA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mazingira wa nchi hiyo Nick Smith amesema kuwa hadi hivi sasa kiwango cha mafuta yaliyovuja kimeongezeka zaidi na kufikia tani 350 baada ya kontena lenye mafuta kuharibika zaidi kufuatia meli hiyo kukumbwa na dhoruba usiku wa leo.

Waziri huyo ameongeza kuwa tukio hilo ambalo limesababisha janga kwa taifa kamwe mamlaka zisingeweza kulizuia kufuatia meli hiyo kugonga mwamba mapema siku ya jumatano
.

Waziri mkuu wa nchi hiyo John Key ambaye alizuru eneo la tukio siku ya jumapili amesema kuwa uchunguzi unafanywa ili kubaini chanzo cha meli hiyo kugonga mwamba.

Waziri mkuu huyo ameongeza kuwa suala la kugonga mwamba unaojulikana katika hali ya utulivu wa maji wakati wa usiku ni jambo la kushangaza ambalo linahitaji kuchunguzwa ili kubaini sababu za tukio hilo.

Kwa upande wake mmiliki wa meli hiyo raia wa Ugiriki Costamare amesema kuwa wanashirikiana kwa karibu na mamlaka husika ili kuzuia na kupunguza athari za mazingira ambazo zimesababishwa na tukio hilo.

Aidha kundi linaloshughulikia wanyama, misitu na ndege limesema kuwa kutokea kwa ajali hiyo katikati mwa msimu wa kuzaliana kwa ndege ni janga kubwa ambalo litaathiri pia viumbe wengine wakiwemo samaki aina ya Dolphine.

Meli ya MV Rena iliyoundwa mwaka 1990 ilikuwa imebeba makontena 1351 ya bidhaa ikiwemo shehena ya mafuta kabla ya kupata ajali siku ya jumapili.