LIBYA

Majeshi ya Baraza la mpito nchini Libya yajipanga kurejesha mashambulizi Sirte.

Majeshi ya Serikali ya Baraza la Taifa la Mpito Nchini Libya NTC yameainisha kujipanga vyema katika kufanya shambulizi jingine ili kufanikiwa kuuchukua Mji wa Sirte baada ya hapo awali kurudishwa nyuma na askari watiifu kwa Kanali Muammar Gaddafi.

Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya,Mustafa Abdejalil
Kiongozi wa Baraza la mpito nchini Libya,Mustafa Abdejalil REUTERS/Esam Al-Fetori
Matangazo ya kibiashara

Makamanda wa NTC wamesema kwa sasa wameshaweka vifaru vyao tayari kwa ajili ya mapambano hayo ambayo wanaamini yatakuwa ya mwisho kabla ya wao kuchukua Mji wa Sirte licha ya uwepo wa upinzani.

Kanali Mohammad Aghfeer amesema wanataka kutekeleza operesheni ya mwisho ambayo itawafanya wauweke chini ya himaya yao Mji wa Sirte eneo ambalo Kanali Gaddafi alizaliwa na anauungwaji mkono mkubwa.

Kauli hizi zinakuja wakati huu ambapo viongozi wa NTC wakisema kupitia satelite wamefanikiwa kubaini Kanali Gaddafi bado yupo nchini Libya na kitu pekee ambacho kimesalia ni muda tu kabla ya kumkamata.

Mapigano ya miezi minane nchini Libya yameshuhudia utawala wa Kanali Muammar Gaddafi ukiwa katika hali ngumu na kuonekena dhahiri kama umepoteza uhalali wake licha ya mwenyewe kuendelea kupambana hasa kule Sirte na Bani Walid.