Ugiriki

Maandamano, migomo vyatikisa Ugiriki, Chile na Yemeni

Reuters/Mohamed al-Sayaghi

Nchi ya Ugiriki imeanza kushuhudia kwa mara nyingine mgomo wa wafanyakazi wa umma ambao utadumu kwa saa 48 ukiwa ni mwendelezo wa kupinga sera ya kubana matumizi ambayo inashinikizwa na serikali ya nchi hiyo.Mgomo huo unahusisha sekta mbalimbali za umma na unatarajiwa kuleta madhara makubwa na kuwaathiri wananchi wa kawaida.

Matangazo ya kibiashara

Mgomo huu unakuja wakati ambapo Wabunge wa nchi hiyo wanatarajiwa kupiga kura kupitisha ubanaji wa matumizi ambao unajumuisha kupunguza wafanyakazi, kupunguza matumizi na kuongeza kodi.

Umoja wa Ulaya, EU na Shirika la Fedha Duniani IMF wamekuwa wakishinikiza mpango huo lakini Gavana wa Benki Kuu nchini Uingereza Sir Mervyn King ameonya juu ya mwenendo wa uchumi wa dunia .

Wakati huohuo kumetokea maandamano makubwa nchini Chile yaliyoambatana na vurugu kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na polisi wakipinga kupanda kwa gharama za elimu ya juu nchini humo.

Wanafunzi hao ambao walijitokeza katika mji wa Santiago walikuwa na mabango kukashifu sera za elimu za serikali yao huku wakichoma moto magari ya polisi pamoja na kuharibu mali nyingine za serikali.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya wanafunzi hao huku ofisi ya rais Sebastian Pinera ikitoa tamko kulaani maandamano hayo ikiwaita wanafunzi hao ni watukutu waliokosa busara.

Wanafunzi wa elimu ya juu nchini humo wamekuwa wakifanya maandamano kushinikiza serikali yao kutoa elimu bure kwa wanafunzi walioko kwenye vyuo vikuu.

Na katika hatua nyingine maelfu ya wananchi nchini Yemen wakiongozwa na mshindi wa tuzo la amani la Nobel Tawakkul Karman wameandamana mjini Sanaa nje ya ofisi za umoja wa mataifa nchini humo wakishinikiza kujiuzulu kwa rais Ali Abdulah Saleh.
Waandamanaji hao walisikika wakisema kuwa wamekwenda kwenye ofisi za umoja huo kushinikiza kuwachukulia hatua rais wao Ali Abdulha Saleh na rais wa Syria Bashar al-Asad waliowaita wahalifu wa kivita na wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu.
Zaidi ya watu saba waliripotiwa kuuawa katika maandamano hayo huku serikali ikiendelea kusisitiza kiongozi wao kutong'atuka madarakani hivi karibuni mpaka pale kipindi cha mpito kitakapomalizika na kufukia makubaliano.
Tume ya haki za binadamu ya umoja wa mataifa kupitia msemaji wake Rupert Colville imelaani mauaji ya wananchi yanayofanywa na vikosi vya serikali.