SYRIA-MAREKANI

Balozi wa Marekani nchini Syria Robert Ford akimbia vitisho vya kutaka kumuua

Balozi wa Marekani Nchini Syria Robert Ford amerejea Washington kutokana na kuhofia usalama wa maisha yake baada ya kupatiwa vitisho kutokana na hatua yake ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na upinzani wanaoshinikiza Rais Bashar Al Assad aondoke madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Kuondoka kwa Balozi Ford nchini Syria kumethibitishwa na Msemaji Msaidizi wa Serikali ya Marekani Mark Toner ambaye amesema kwa hatua ambayo imefikia wameona ni vyema kwa Balozi huyo akarejea Washington kwa usalama wake.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Balozi Ford baada ya kurejea Washington amepewa likizo yote hiyo ikiwa ni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa maisha yake unakuwa wa hali ya juu kutokana na kuandamwa na vitisho.

Balozi Ford aliingia kwenye ukosaji mkubwa kutoka Damascus baada ya kuonekana akiunga mkono harakati za wapinzani kitu ambacho kiliwasukuma wafuasi wa Rais Assad kumpiga na maganda ya mayai kuonesha hasira zao.

Serikali ya marekani licha ya kumrejesha nyumbani Balozi Ford imeendelea na msimamo wake wa kuutaka Utawala wa Rais Assad kuhakikisha wanafanya mabadiliko ikiwemo ni pamoja na kuruhusu demokrasia kuchukua mkondo wake.

Upinzani nchini Syria umekuwa mstari wa mbele kushinikiza mabadiliko licha ya kuendelea kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya serikali kitu ambacho kimetoa dosari Utawala wa Rais Assad.

Marekani kupitia Rais Barack Obama na hata Waziri wake wa Mambo ya Nje Hillary Clinton mara kadhaa wamenukuliwa wakisema utawala wa Rais Assad umepoteza uhalali wa kuongoza lakini wenyewe wameendelea na msimamo wao wa kudhibiti maandamano.

Takwimu za Umoja wa Mataifa UN zinaonesha kuwa watu zaidi ya elfu tatu wamepoteza maisha tangua kuanza kwa vuguvugu la kutaka kuondoka madarakani kwa Rais Assad pamoja na wafuasi wake.