LIBYA

Mwili wa Kanali Muammar Gaddafi wazikwa pamoja na wenzake wawili

Kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi, Mtoto wake Muatassim Gaddafi pamoja na Mshirika wa karibu wa Kiongozi huyo wamezikwa kwa siri katika eneo la jangwa ambalo halijaainishwa kwa umma.

Matangazo ya kibiashara

Maofisa wa Baraza la Mpito la Taifa NTC wamethibitisha kuzikwa kwa Kanali Gaddafi na wenzake wawili ambao waliuawa baada ya kukamatwa katika Jiji la Sirte mapema siku ya alhamisi ya juma lililopita.

Mazishi hayo yamefanyika kwa siri kama ambavyo NTC walivyoahidi na wamekataa kuanisha sehemu ambayo mwili wa Kanali Gaddafi na wenzake imepumzishwa kutokana na kutohitaji watu wajue eneo hilo na kwenda kuzuru.

Mmoja wa Viongozi wa NTC Guma Al Gamaty amethibitisha kuzikwa kwa Kanali Gaddafi na wenzake wawili siku kadhaa baada ya mwili wake kuanikwa kwenye chumba maalum ambacho kiliwapa watu nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.

Familia ya Kanali Gaddafi ilomba ipatiwe mwili wa Kiongozi huyo kwa ajili ya taratibu za mazishi kitu ambacho kilipigwa na NTC ambao walijiapiza kuzika wenyewe mahali ambapo patasalia kuwa siri.

Miili hiyo ilihifadhiwa katika chumba kimoja huko Misrata tangu kutokea kwa vifo vyao mnamo siku ya alhamisi huku Jumuiya ya kimataifa ikishinikiza uchunguzi ufanywe kubaini namna ambavyo kifo hicho kilitokea.

Hiyo jana Kiongozi wa Libya Mustafa Abdel Jalil aliithibitishia dunia kuwa atahakikisha kunaundwa Tume Maalum ambayo itafanya uchunguzi wa kubaini kifo cha Kanali Gaddafi kilivyotokea.

Kiongozi wa Libya Jalil siku ya jumapili alitangaza ukombozi wa Taifa hilo ambao umekuja baada ya makabiliano makali ambayo yalisaidiwa na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO yalidumu kwa miezi tisa kabla ya kuuawa kwa Kanali Gaddafi.