LIBYA-MAREKANI-UFARANSA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kupiga kura kuamua hatima ya Majeshi ya NATO huko Libya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN linatarajiwa baadaye alhamisi kupiga kura kuamua iwapo operesheni ya Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO iliyofanyika nchini Libya kufanikisha kuanguka kwa Utawala wa Kanali Muammar Gaddafi ifikie tamati tarehe 31 ya mwezi Oktoba au la.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ndiyo ambayo imethibitisha Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kuwa na jukumu la kupiga kura kuamua mwisho wa operesheni ya Majeshi ya NATO huko Libya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Ufaransa Bernard Valero amewaambia waandishi wa habari ya kwamba wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN watakuwa na jukumu la kupitisha azimio jipya la kumaliza muda wa Majeshi ya NATO kuwepo Libya ambalo litabadilisha azimio namba 1973.

Uamuzi huu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kupiga kura kuamua kumaliza operesheni ya Majeshi ya NATO nchini Libya unakuja wakati ambapo hiyo jana Mustafa Abdel Jalil akitaka kiurefushwa kwa muda zaidi kwa majeshi hayo kuwepo nchini mwake.

Haya yanakuja wakati huu ambapo kuna taarifa Mkuu wa Usalama wa Taifa wakati wa Utawala wa Kanali Gaddafi, Abdullah Al Senussi ambaye anasakwa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ICC akishukiwa ameondoka nchini Niger na kueleka Mali.

Taarifa kutoka kwa vyanzo vya uhakika wa habari zinathibitisha Al Senussi ambaye alikuwa nchini Niger amekimbilia katika Jangwa la Mali kwa lengo la kusaka hifadhi baada ya kuangushwa kwa utwala wao.

Taarifa hizo hazijaainisha kama Mtoto wa Kanali Gaddafi, Seif Al Islam naye ameeleka Mali baada ya kuwepo kwa uvumi yupo tayari kujisalimisha kwenye Mahakama ya ICC kuliko kurejea nchini Libya ambako Utawala mpya umeshatangaza ukombozi wa taifa hilo.

Senussi pamoja na Seif Al Islam wanasakwa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ICC tangu tarehe ishirini ya mwezi Juni mwaka huu ilipotolewa waranti ya kukamatwa kwao kutokana na kukabiliwa na makosa ya uhalifu wa kivita.