Libya-ICC

Mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi Seif al Islam awasiliana na mahakama ya ICC

Seif al-Islam Gaddafi
Seif al-Islam Gaddafi Tunisienews

Kiongozi wa mashtaka wa mahakama ya Uhalifu wa kivita ya Kimataifa, ICC Louis Mereno Ocampo anasema mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi, Seif al Islam, anajitetea kuwa hana makosa. Seif Gaddafi amejificha, baada ya serikali ya baba yake kuangushwa madarakani na kuuawa kwake.

Matangazo ya kibiashara

Luis Moreno-Ocampo anasema Saif Al Islam kwa kupitia wajumbe, amemwambia kuwa anataka kufutiwa mashtaka, anayotuhumiwa kuyafanya kwa kusababisha mauaji ya raia nchini Libya.

Aidha Ocampo amesema, Saif Gaddafi amekuwa na hamu ya kutaka kujua hatima yake, endapo ICC itamkuta hana makosa.

Seif Al Islam anakanusha kuwa aliamrisha mashambulizi ya mabomu na risasi dhidi ya waandamanaji nchini Libya, wakati maandamano yalipoanza nchini Libya mapema mwaka huu, na anasema anaweza kutoa ushahidi kuonesha kuwa hana hatia.

Mahakama ya ICC imemshtaki Saif Gaddafi, hayati baba yake, Kanali Gaddafi, na mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi Abdullah al-Senussi, kwa uhalifu wa kivita.

Ocampo anataka kumfikisha the Hague mtoto wa hayati kanali Gaddafi ili kuanza kesi.