UFARANSA-PARIS

UNESCO yapiga kura ya ndio kukubali nchi ya Palestina kuwa mwanachama wake wa kudumu

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa kauli moja hii leo wajumbe wake wamepiga kura kukubali kuipa uwanachama wa kudumu katika shirika hilo nchi ya Palestina.

UNESCO
UNESCO Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mataifa mia moja na sabini na tatu wanachama wa Shirika hilo walipiga kura ambapo wajumbe mia moja na saba walisema ndio kwa Palestina kupewa uanachama wa kudumu wakati wajumbe kumi na nne walipinga nchi hiyo kupewa uwanachama.

Miongoni mwa nchi ambazo zilipiga kura ya hapana katika kikao hicho kilichofanyika mjini Paris Ufaransa ni pamoja na Israel, Marekani, Canada, Australia na Ujerumani wakati nchi za Japan na Uingereza zenyewe hazikupiga kura.

Hatua ya Shirika hilo kukubali kuipa uanachama wa kudumu nchi ya Palestina imezusha maswali mengi ambapo nchi ya Marekani ilitangaza hadharani kuwa itasitisha msaada wake wa fedha kwenye shirika hilo kwa zaidi ya aslimia 22.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, balozi wa Palestina katika umoja wa mataifa Riyad al-Malki amesema kuwa hatua hiyo ya UNESCO kukubali kuipa uanachama wa kudumu ni ushindi tosha kwa nchi yake na kwamba wanauhakika nchi yao itapewa uanachama huo katika kikao cha Baraza la Usalama.

Hata hivyo ni Baraza la Usalama pekee ndilo linalosubiriwa kutoa maamuzi iwapo litakubali kuipa uanachama Palestina au la, jambo ambalo hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa huenda lisitokee kwakuwa nchi ya Marekani, China, Urusi na Ujerumani walishapinga toka awali.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinatarajiwa kuketi mwezi wa kumi na moja mwaka huu kuamua hatma ya Palestina.