UFARANSA

Ujerumani na Ufaransa yatoa makataa kwa Ugiriki kuamua kama inataka kubaki kwenye Umoja wa Ulaya au la

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy Reuters

Viongozi wa nchi za Ujerumani na Ufaransa wametoa makataa kwa nchi ya Ugiriki na kusema kuwa nchi hiyo haitapatiwa msaada wowote wa kifedha toka kwenye umoja huo mpaka pale itakapoamua endapo inataka kubakia au la.

Matangazo ya kibiashara

Wakizungumza na waandishi wa habari kusinini mwa nchi ya Ufaransa katika mji wa Cannes unakofanyika mkutano wa viongozi wa nchi 20 tajiri za viwanda duniani, rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na kansela wa Ujerumani Angela Markel wamesema kuwa ni lazima jirani zao hao waamue kama wanataka kubakia kwenye umoja huo au la.

Juma moja lililopita rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy aliweka wazi msimamo wa nchi yake na kusema kuwa Umoja wa Ulaya ulifanya makosa sana kuipa uanachama nchi ya Ugiriki kabla ya kuichunguza vizuri akiituhumu kuwa ndio iliyochangia pakubwa katika mdororo wa uchumi ulioko duniani hivi sasa.

Katika mkutano huo wa nchi 20 tajiri za viwanda dunini pia unahudhuriwa na waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou ambaye siku ya jumatatu alitangaza nchi yake kuitisha kura ya maoni kuamua nchi hiyo kama iendelee kubakia kwenye Umoja huo ama kujitoa.

Kauli yake iliungwa mkono na baraza la mawaziri ingawa wapo hata wabunge wa chama chake waliopinga shauri lake ambapo kura hiyo ya maoni inatarajiwa kupigwa hapo kesho kuamua hatma yao.

Katika mkutano huo unaofanyika nchini Ufaransa waziri mkuu Papandreou anatarajiwa kuhutubia viongozi wa mataifa mengine ya dunia ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuayashawishi mataifa hayo kuendelea kuwa na imani na nchi yake kwa kuipatia fedha pamoja na kwenda kuwekeza nchini mwake.

Mkutano huo pia unatarajiwa kujadili halo ya mgogoro wa kiuchumi ulioyakumba mataifa ya Ulaya na Amerika na namna ambavyo nchi hizo zinaweza kutoa msaada kunusuru mataifa mengine kutumbukia katika mdororo wa uchumi.