UGIRIKI-ATHENS

Waziri mkuu wa Ugiriki akabiliwa na kura ya kutokuwa na imani nae

Waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou akizungumza wakati wa kikao cha baraza la mawaziri hapo jana
Waziri mkuu wa Ugiriki, George Papandreou akizungumza wakati wa kikao cha baraza la mawaziri hapo jana Reuters

Waziri mkuu wa Ugiriki George Papandreou amesema kuwa ataahirisha mpango wake wa kuitisha kura ya maoni juu ya mkopo kutoka umoja wa ulaya na mashirika ya fedha duniani na kusema kuwa atafanya mazungumzo na upinzani ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa na kiuchumi nchini humo..

Matangazo ya kibiashara

Katika hotuba yake kwa baraza la mawaziri hapo jana Papandreou amesema ataanzisha mazungumzo na upinzani, huku akisifu kuwa uungwaji mkono wa hatua yake hiyo ni muhimu.

Waziri mkuu huyo amesema ikiwa upinzani utaridhia pendekezo lake kupelekwa bungeni kura ya maoni haitapigwa nchini humo Papandreau amesema kuwa atafurahi ikiwa hawatafikia hatua ya kupiga kura ya maoni na anafurahi kuwa hivi sasa majadiliano ya mara kwa mara angalau yamewafanya watu wa ugiriki waanze kumuelewa.

Akizungumza na bunge la nchi hiyo Papandreau ameshukuru upinzani kwa kubadili mawazo juu ya mkopo huo na halikadhalika ameahidi kuzungumza na kiongozi wa upinzani ili waweze kufanya tathmini za hatua zinazofuata ili kufukia muafaka.

Papandreau alipewa sharti na mataifa yenye nguvu ya G20 mjini CANNE nchini ufaransa kuwa ugiriki inapaswa kuchagua ikiwa inataka kuendelea kubaki kuwa mwanachama anayetumia sarafu ya Euro au nchi hiyo ikose mkopo huo.

Waziri mkuu huyo hii leo anakabiliwa na kura ya kuwa na imani nae ama la,hatua ambayo pengine inaweza kumfanya kuendelea kutumikia wadhifa wake huo ama la.

Usiku wa hii leo bunge la nchi hiyo litapiga kura ya kuwa na imani au la na waziri mkuu Papandreou ambae huu ni mtihani mwingine anaopaswa kufaulu endapo anataka kubakia marakani.