Saudi Arabia-Hijja

Mamilioni ya mahujaji kutoka kona tofauti wamiminika kwenye mlima Arafa kutekeleza ibada ya Hijja

Ibada ya Hijja
Ibada ya Hijja

Zaidi ya mahujaji milioni tatu, wakiwa wamevalia nguo nyeupe, wanaendelea kumiminika kwenye viwanja vya Mlima Arafat hivi sasa, ikiwa ni sehemu muhimu ya ibada yao ya Hijja. Inaripotiwa kuwepo hali ya usalama wa kiwango cha juu.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia, Mansour Al-Turki, amesema kwamba kila kitu kinakwenda kama kilivyotegemewa, na kwamba hakuna kitisho chochote kwa usalama wa mahujaji, wala kwa nchi.

Katika miaka iliyopita, kulikuwa na matukio yanayohatarisha usalama kwenye ibada hii, hasa kutokana na msongomano mkubwa wa watu, vurugu na moto. Mwaka 1987, mahujaji wa Iran waliandamana, na kusababisha ghasia zilizomalizika kwa vifo vya watu 400. Mwaka 2006, mahujaji 346 wa mataifa tafauti walikufa, baada ya msongomano katika tukio la kurusha mawe kwenye mnara, kama ishara ya kumlaani Ibilisi.

Mlima wa Arafat ni sehemu ambapo kiongozi wa umma wa Kiislamu, Mtume Muhamad (S.A.W), alitoa hotuba yake ya mwisho kwa wafuasi wake, karne 14 zilizopita. Hijja ni nguzo ya tano katika Uislamu, ambayo humlazimu kila muumini mwenye uwezo kuitekeleza, angalau mara moja maishani mwake.