BENIN

Papa Benedict XVI atoa onyo kwa viongozi wa Afrika

© Reuters/Stefano Rellandini

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedict wa 16 ametoa onyo kwa viongozi wa bara la Afrika kuepuka rushwa na kuacha kuwaibia wananchi ili kuepuka vurugu na uvunjifu wa amani.

Matangazo ya kibiashara

Kiongozi huyo ameyasema hayo alipotembelea nchi ya Benin kwa ziara ya siku tatu iliyoanza hapo jana,ambapo amepokelewa kwa shangwe na maandamano kutoka kwa waumini wa kikatoliki nchini humo.

Papa Benedict wa 16 amesema kuwa amechagua kuitembelea nchi ya Benin katika ziara yake ya pili barani Afrika kwa kuwa anaamini kuwa ni nchi ambayo imekuwa na amani kati ya waumini wa kikristo,waislam na waumini wa dini za jadi.

Wakati akiingia katika kanisa kuu la mjini Cotonou Papa Benedict wa 16 amesikika akiwaombea waathirika wa vita, wakiwemo watoto na vijana wenye kiu ya haki na mapatano yenye kuleta amani barani Afrika.

Ziara ya kiongozi huyo inakuja wakati bado masuala ya ukosefu wa haki,rushwa,ulafi na vurugu zikijitokeza katika maeneo mbalimbali barani Afrika jambo linalosababisha watu kupata taabu katika nchi zao.