MISRI-TAHRIR

22 wathibitishwa kufa katika machafuko yanayoendelea nchini Misri

Waandamanaji wa Misri wakikabilina na polisi
Waandamanaji wa Misri wakikabilina na polisi Reuters

Maandamano nchini Misri ya kupinga utawala wa kijeshi nchini humo yameendelea kwa siku ya tatu mfululizo hii leo ambapo waandamanaji wamefanikiwa kurejea tena kwenye uwanja wa Tahriri wakiitisha mkusanyiko mkubwa kupinga serikali.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa kutoka nchini humo zinasema kuwa zaidi ya watu ishirini na mbili mpaka sasa wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya mia moja wamejeruhiwa kufuatia polisi wa kutuliza ghasia hapo jana a juzi kujaribu kuingia katika uwanja wa Tahriri kuwatawanya waandamanaji hao.

Maandamano hayo abayo yalianza siku ya Ijumaa yameshuhudiwa yakienea pia hadi katika miji mingine kama ya Alexandria, Al-Minya na Suez ambako wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi.

Wananchi hao wanataka kufikia tamati kwa utawala wa kijeshi nchini humo wakiushinikiza kurejesha utawala wa kiraia suala ambalo bado limeonekana kuwa gumu kutekelezwa na serikali ya kijeshi.

Waandamanaji hao wameituhumu mahakama kuu ya nchi hiyo kwa kuruhusu baraza la kijeshi nchini humo kuendelea kusalia madarakani mpaka utakapoitishwa uchaguzi mkuu hapo mwakani au mwaka wa 2013 mwezi wa kwanza kitu ambacho wananchi hao wanakipinga na kutaka serikali ya mpito.

Kiongozi wa baraza hilo ameelezea kusikitishwa kwake na vifo vilivyotokea na kuendelea kusisitiza kusalia madarakani hata mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika November 28 mwaka huu.

Wachambuzi wa mambo wanaonya kuwa vurugu hizo huenda zikasababisha maafa zaidi nchini humo endapo viongozi hao hawatakutana na baraza la kijeshi kukubaliana kuhusu uundwaji wa serikali ya mpito.