MANAMA-BAHRAIN

Ripoti ya uchunguzi kuhusu mauaji ya raia nchini Bahrain yatolewa

Baadhi waandamanaji nchini Bahrain walipoandamana hivi karibuni kupinga utawala wa nchi hiyo
Baadhi waandamanaji nchini Bahrain walipoandamana hivi karibuni kupinga utawala wa nchi hiyo Reuters

Polisi nchini Bahrain wamelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya maelfu ya wananchi walioandamana katika mji wa Manama wakipinga kitendo cha askari kutumia nguvu kubwa kuwatawanya waandamanaji.

Matangazo ya kibiashara

Wakati kukitokea machafuko hayo mapya, ripoti maalumu ya uchunguzi ulioagizwa kufanywa na mfalme wa nchi hiyo Hamad Bin Isa al Khalifa imekabidhiwa na kusomwa mble ya mfalme huyo huku ikibainisha utumikaji mkubwa wa nguvu wakati wa kuwatawanya wananchi kwenye maandamano ya mweizi wa kwanza na wa pili mwaka huu.

Mfalme al-Khalifa aliunda tume huru mwezi wa sita mwaka huu na kuagiza uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu mauaji ya raia yanayodaiwa kufanywa na polisi pamoja na tuhuma kuwa kulikuwa na unyanyasaji mkubwa wa raia waliokuwa wakikamatwa na polisi.

Tume hiyo ambayo leo ndio imewasilisha ripoti hiyo mbele ya mfalme, imeeleza kwa kina jinsi ilivyofanya uchunguzi wake na kwamba ni kweli polisi walitumia nguvu kubwa kuwatawanya waandamanaji na kusababisha vifo vya raia wengi wakiwemo wanaharakati.

Ripoti hiyo pia imesema kuwa hakuna uhusiano wowote wa maandamano hayo na nchi ya Iran ambayo ilitajwa kufadhili mtandao wa makundi ya watu ambao walikuwa wakihamasisha migomo na maandamano.

Tume hiyo pia imebainisha kuwa wanaharakati pamoja na raia ambao wanashikiliwa bado kwenye magereza ya nchi hiyo wanafanyiwa vitendo vya unyanyasaji na kuitaka serikali kuingilia kati kwa kuwaachia huru watu hao kwa lengo la kuzuia machafuko mapya kutokea.

Mfalme Hamad Bin Isa al-Khalifa akihutubia viongozi wa Serikali, amesema kuwa kuna haja ya nchi hiyo kufanyia mabadiliko sheria zake ili ziendane na wakati akisistiza kuwa atafanya hivyo bila shinikizo lolote toka kwa jumuiya ya kimataifa.

Mbali na kuahidi kufanya mabadiliko ya sheria za nchi, kiongozi huyo ametumia hotuba yake kuwatuhumu wanaharakati na watu aliowaita makundi ya kigaidi kwa kuchochea machafuko nchini humo hali iliyosababisha polisi kutumia nguvu zaidi.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa wakati nchi hiyo ikijiandaa kufanya mabadiliko katika sheria za nchi ni lazima sheria mpya zitakazotungwa ziendane na kulingana na matakwa ya wananchi wote na sio kwa upendeleo.

Mfalme al-khalifa ameahidi kuwachukulia hatua viongozi wote ambao wametajwa kwenye ripoti hiyo na kwamba walihusika kwa namna moja ama nyingine katika kuamrisha mauaji ama unyanyasaji wa wananchi waliokuwa wamekamatwa.