MISRI-MAREKANI

Utawala wa Kijeshi Nchini Misri upo tayari kukabidhi madaraka kwa Utawala wa Kiraia baada ya Uchaguzi wa Rais

Utawala wa Kijeshi nchini Misri chini ya Field Marshal Mohammed Hussein Tantawi umekubali kukabidhi madarakani kwa serikali ya kiraia punde tu baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa Rais hapo mwakani mwezi wa Juni.

Matangazo ya kibiashara

Field Marshal Tantawi amesema Utawala wake hauna lengo la kung'ang'ania kukaa madarakani kama ambavyo waandamanaji wamedai badala yake inataka kusimamia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa rais hapo mwezi Juni mwakani.

Kiongozi wa Utawala wa Kijeshi Tantawi amesema kwa kudhihirisha hilo serikali yake itasimamia kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika tarehe ishirini na nane ya mwezi huu kama ilivyo.

Tantawi amesema wananchi wanatakiwa na imani na Utawala huo ambao pia upo tayari kuhakikisha unasimamia kura ya maamuzi juu ya kupatikana kwa katiba mpya ambayo itatoa demokrasia kwa wananchi.

Field Marshal Tantawi pia amesema serikali yake imekubali uamuzi wa kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Essam Sharaf na Baraza lake la Mawaziri kwa lengo la kusitisha machafuko yaliyojitokeza mwisho mwa juma lililopita.

Kauli hii inakuja wakati ambapo machafuko mpya yaliyoibuka nchini Misri yakiingia katika siku yake ya sita huku idadi ya vifo ikiwa ni watu thelathini na wanne baada ya mtu mwingine mmoja kupoteza maisha hapo jana.

Serikali ya Marekani yenyewe imejitokea na kulaani vikali machafuko ambayo yamezuka nchini Misri kwa sasa na kusababisha vifo vya waandamanaji ambao wanataka uwepo wa Utawala wa Kiraia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani Victoria Nuland amesema nchi yake inataka kuona madai ya waandamanaji waliofanikisha mapinduzi ya mwezi february yanasikilizwa mara moja na ipatikane serikali ya kiraia.

Kwa upande wao waandamanaji ambao wamepiga kambi katika viunga vya Tahrir wamesema kauli hiyo ya Field Marshal Tantawi haisaidii chochote na badala yake wataendelea na shinikizo lake kumtaka yeye na Utawala wake wa Kijeshi uondoke.

Waandamanaji nchini Misri ndiyo ambao walifanikisha kuangushwa kwa serikali ya Rais Hosni Mubarak mnamo mwezi february na kisha nchi hiyo ikawa chini ya serikali ya mpito inayoongozwa na jeshi.