Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa watoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Kidemokarasia ya Kongo kupiga kura kwa amani

RFI/Anthony Terrade

Wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanapiga kura kumchagua rais na wabunge Jumatatu hii,katika uchaguzi wa pili wa kidemokrasia nchini humo,katika taifa hilo ambalo limekuwa likitawaliwa na vita vya muda mrefu.

Matangazo ya kibiashara

Wagombea 11 wanawania kiti cha urais akiwemo rais wa sasa Joseph Kabila ambaye anatarajia upinzani mkali kutoka kwa  mpinzani wake mkuu Etienne Tshisekedi.
 

Zaidi ya wagombea elfu kumi na wanane pia wanawania nyadhifa za ubunge,kutaka kuchaguliwa katika bunge la kitaifa la wabunge 500 .
 

Licha ya changamoto za hapa na pale za kusafisha makaratasi ya kupigia kura kutokana na miundo mbinu mibovu nchini humo,tume ya uchaguzi nchini humo CENI inasema kuwa kila kitu kiko tayari na sasa kinachosalia ni kwa wananchi wa DRC kutimiza haki yao ya kidemokarasia.
 

Katibu Mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amewataka wananchi wa DRC kuwa watulivu wakati huu wa uchaguzi na kupiga kura kwa amani,na kutoa wito kwa serikali kuhakisha kuwa inawalinda raia wake.
 

Wito huo unatolewa baada ya kufariki kwa watu wawili katika jiji la Kinshasa siku ya Jumamosi,baada ya makabiliano kuzuka kati ya polisi na wafuasi wa upinzani baada ya polisi kusitisha kampeni za kisiasa jijini humo kwa sababu za kiusalama.
 

Uamuzi huo wa polisi ulisababisha mapambano kati ya wafuasi wa kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi na kusabisha vifo hivyo huku wengine wakijeruhiwa,na Tshisekedi mwenyewe kuzuiliwa katika uwanja wa ndege.
 

Uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemorsaia ya Kongo unaangaziwa kwa umakini mkubwa na jamii ya kimataifa na tayari,mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC imeonya kuwa yeyote atakayesababisha machafuko nchini humo wakati wa kipindi cha uchaguzi na baada ya uchaguzi atachukuliwa hatua za kisheria.