Congo

Zoezi la upigaji kura katika jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo laanza vyema

Kituo cha kupigia kura nchini DRC katika maeneo ya Goma
Kituo cha kupigia kura nchini DRC katika maeneo ya Goma RFI, LUKUMBUKA, GOMA

Wananchi zaidi ya milioni thalathini na tatu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanapiga kura kumchagua rais na wabunge leo Jumatatu, katika uchaguzi wa pili wa kidemokrasia nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Wagombea 11 wanawania kiti cha urais akiwemo rais wa sasa Joseph Kabila ambaye anatarajia upinzani mkali kutoka mpinzani wake mkuu Etienne Tshisekedi.

 Zaidi ya wagombea elfu kumi na nane pia wanawania nyadhifa za ubunge,kutaka kuchaguliwa katika bunge la kitaifa la wabunge 500 .
 

Maafisa wa tume ya uchaguzi nchini humo CENI wanasema kuwa zoezi hilo linaendelea vema katika vituo vyote elfu 60 vya kupigia kura,licha ya changamoto za kusafirisha vifaa na marakatasi ya kupigia kura kushuhudiwa hapo awali kutokana na miundo mbinu mibovu.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa kumi na mbili kamili asubuhi saa za Afrika ya Kati na, vinatazamiwa kufungwa saa kumi mchana.
 

Jumamosi iliyopita machafuko yalizuka mjini Kinshasa kati ya polisi na wafuasi wa upinzani na kusabisha kufariki kwa watu wawili na wengine kujeruhiwa .

Umoja wa mataifa pamoja na jumuiya ya Ulaya unatoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Kongo kudumisha amani wakati huu wanapotekeleza zoezi hilo la upigaji kura na pia kusalia vivyo hivyo baada ya matokeo ya uchaguzi huo.