SYRIA

Umoja wa Mataifa wavishutumu Vikosi vya Syria kuhusika na vitendo vya uhalifu dhidi ya Ubinaadam

(REUTERS)

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaofanya uchunguzi juu ya mauaji ya nchini Syria,umesema kuwa vikosi vya usalama nchini Syria vimejihusisha na vitendo vya uhalifu dhidi ya ubinaadam ikiwemo mauaji na kutesa watoto.

Matangazo ya kibiashara

Wakati waziri wa mambo ya nje wa Syria, Walid Muallem akionesha wanahabari picha za video zikionesha picha za kaburi la pamoja la vikosi vya usalama, mjini Geneva nchini Uswisi ripoti ya umoja wa mataifa imeshutumu vitendo viovu vya majeshi ya utawala.

Wachunguzi kutoka tume huru ya uchunguzi juu ya Syria imewashutumu maafisa wa serikali kuhusika katika vitendo vya mauaji, ubakaji na utesaji wakati walipokuwa wakidhibiti waandamanaji tangu mwezi March mwaka huu, halikadhalika wamemlaumu kiongozi wa taifa hilo Bashar Al Assad kutoa Amri ya utekelezaji.

Jopo hilo liliwahoji waathiriwa 223 na mashuhuda wakiwemo wanajeshi walioasi jeshi la Assad ambao walikuwa wakipewa Amri ya kutekeleza vitendo vya mauaji dhidi ya waandamanaji.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Paulo Pinheiro amesema vikosi vya Assad vimeshiriki katika vitendo vya ukiukwaji wa ubinaadam katika vitendo vya ukandamizaji wa raia waliokuwa wakiandamana kwa amani.
 

Katika hatua nyingine, Damascus imeushambulia kwa maneno umoja wa nchi za kiarabu kwa kufumbia macho taarifa za uwepo wa Magaidi nchini Syria na uamuzi wake wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.