AFGHANISTAN-PAKISTAN-UJERUMANI

Mkutano wa kujadili mustakabali wa nchi ya Afghanistan wafanyika huko Ujerumani

Reuters

Mkutano wa Kimataifa wa kujadili hatima ya Afghanistan unaanza rasmi leo nchini Ujerumani katika Jiji la Bonn licha ya mshirika muhimu kwenye mazungumzo hayo nchi ya Pakistan kususia mkutano huo.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huu unawaleta pamoja wajumbe kutoka nchi mia moja na Mashirika ya Kimataifa ambayo yatakuwa na jukumu moja muhimu la kujadili namna ambavyo wanahakikisha nchi ya Afghanistan inastawi.

Pakistan imesusia mkutano huo kwa sababu moja kubwa ambayo ni kutokana na kuendelea kutekelezwa kwa mashambulizi ya Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO ambayo yamekuwa yakisababisha vifo kila kukicha.

Serikali ya Pakistan imekuwa ikishinikiza Marekani na Majeshi ya NATO kuomba radhi kutokana na mashambulizi yake ambayo yamesababisha vifo vya watu ishirini na nne hatua ambayo imepingwa na taifa hilo.

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai amesema huu ni mkutano muhimu sana kwa nchi hiyo ambao unaweza kuibuka na mkakati wa kuweza kuisaidia kupiga hatua za kimaendelea baada ya machafuko ya muda mrefu.

Marekani inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinto ambaye anatarajiwa pia kukutana na Rais Karzai kujadili tarehe ya kuondolewa kwa Majeshi ya NATO ambayo yanashika doria kwa sasa.

Majeshi ya NATO ambayo yanashika doria nchini Afghanistan yanatakiwa yameondoka kufika mwaka elfu mbili kumi na nne na kwa sasa wameendelea kukubaliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na kuchangia ongezeko la vifo kupitia mashambulizi yake.

Pakistan imesusia mkutano huo licha ya umuhimu wake katika kuhakikisha wanafanikisha kumaliza nguvu waliyonayo Kundi la Wanamgambo wa Taliban linalopambana na serikali kwa hali ya juu.

Mkutano huu unakuja ikiwa ni miaka kumi tangu kuangushwa kwa Utawala wa Kundi la Taliban ambalo lilikuwa linatawala nchi hiyo na kufuatia na machafuko baada ya Marekani chini ya mwamvuli wa NATO kuingia katika nchi hiyo.