IRAQ-MAREKANI

Katibu Mkuu wa NATO atangaza majeshi yake kuondoka Nchini Iraqi mwishoni mwa mwaka huu

Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO kupitia Katibu Mkuu wake Anders Fogh Rasmussen imetangaza mwisho wa mwaka huu ndiyo watamaliza mpango wao wa kutoa mafunzo kwa vikosi vya ulinzi vya Iraqi.

Matangazo ya kibiashara

Rasmussen ametoa tamko hilo hii leo na kusema kuwa wanajeshi wa NATO watamaliza kibarua chao cha kutoa mafunzo mnamo tarehe thelathini na moja ya mwezi Desemba mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na NATO kupitia Katibu Mkuu Rasmussen imesema majeshi yao hayataendelea kuwepo Iraqi baada ya tarehe hiyo na hivyo watakuwa wametamatisha jukumu la kutoa mafunzo.

Mshauri wa Ulinzi wa Iraqi Falah Al Fayadh naye amethibitisha kufikiwa kwa makubaliano ya kuondoka kwa majeshi ya NATO nchini humo itakapofika tarehe ya mwisho ya mwaka 2011.

Katibu Mkuu wa NATO ameongeza kwenye taarifa yake kuwa hakuna makubaliano yoyote ya kuongeza muda kwa majeshi yao kuendelea kusalia nchini Iraqi.

Tamko hili linakuja wakati huu ambapo Waziri Mkuu wa Iraqi Nuri Al Maliki akiwa ameelekea nchini Marekani kukutana na Rais Barack Obama kujadili tarehe ya kuondoka kwa majeshi ya nchi hiyo yanayoshika doria nchini mwake.

Mazungumzo ya viongozi hayo yanatarajiwa kutawalia na namna ambavyo wanajeshi hao watakapoondoka na suala la ulinzi litakavyobaki kwa wanajeshi wa Iraqi.

Marekani inawajeshi wake wanaofikia elfu sita nchini Iraqi wakiwa na jukumu kubwa la kuhakikisha wanashika doria na kutoa mafunzo kwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.

Uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Iraqi ni matokeo ya kuangushwa kwa Utawala wa Marehemu Saddam Hussein baada ya kufanyika kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani pamoja na washirika wao Uingereza kusaka silaha za maangamizi.