IRAQ-MAREKANI

Marekani yakubali kuondoa Majeshi yake nchini Iraq mwishoni mwa mwaka huu

REUTERS/Jonathan Ernst

Serikali ya Marekani nayo imeungana na uamuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO wa kuondoa majeshi yake nchini Iraqi mwishoni mwa mwaka huu na kukabidhi rasmi jukumu hilo kwa Vikosi vya Taifa hilo.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani Barack Obama ndiyer ambaye ametangaza uamuzi huo wakati alipokutana na Waziri Mkuu wa Iraqi Nouri Al Maliki kwa ajili ya kujadili hatima ya maesji ya Marekani ambayo yanashika doria na kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi yake.

Rais Obama amesema tukio la kuondoa wanajeshi wao ambao wanafikia elfu sita nchini Iraqi ni la kihistoria na linakuja baada ya wao kukamilisha kazi ya kuungoa utawala wa Rais wa zamani Marehemu Saddam Hussein na washirika wake.

Kiongozi huyo wa Marekani amepongeza pia juhudi ambazo zimefanywa na Waziri Mkuu Al Maliki na kusema zimefanikisha pakubwa kwa majeshi ya nchi yake kuweza kutekeleza jukumu lake la kushika doria katika nchi hiyo.

Rais Obama amesisitiza majeshi yake yanaondoka nchini Iraqi kwa heshima huku wakijivunia kile ambacho wamekifanya kwa wananchi wa taifa hilo tangu walipoingia mwaka 2003 wakishirikiana na Uingereza kuuangusha Utawala wa Saddam Hussein.

Marekani imetangaza kuwa huu ni mwisho rasmi wa vita ambavyo vilikuwa vinashuhudiwa nchini Iraqi ambavyo vilikuwa vinakwenda sambamba na matukio ya kujitoa mhanga kwenye nchi hiyo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Al Maliki amesema nchi yake itaendelea kuhitaji msaada wa kitaaluma kutoka kwa mataifa ya nje ili iweze kupiga hatua kwenye nyanja za kisiasa, kiuchumi na kielimu.

Al Maliki pia amewaonya majirani zao ambao wamekuwa mstari wa mbele kutaka nchi hiyo isiwe na utulivu waache kufanya hivyo na badala yake wasaidie kupatikana utulivu wa kweli kwenye nchi hiyo.

Marekani ilikuwa na jumla ya wanajeshi laki moja na elfu sabini nchini Iraqi lakini ilianza kuwapunguza pale ambapo shinikizo la kuwataka waondoke lilipoanza na sasa wamesalia elfu sitini pekee.