RWANDA-DRC

Mahakama ya ICC yamwachia huru kiongozi wa waasi wa Rwanda

Kiongozi wa kundi la FDLR la Rwanda Callixte Mbarushimana
Kiongozi wa kundi la FDLR la Rwanda Callixte Mbarushimana DR

Majaji katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC wametupilia mbali mashitaka dhidi ya kiongozi wa waasi wa nchini Rwanda Callixte Mbarushimana ambaye alikuwa akituhumiwa kwa kufanya uhalifu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuagiza muasi huyo kuachiwa huru.

Matangazo ya kibiashara

Jopo la majaji hao wakiongozwa na jaji Sanji Mmasemono Monageng wameagiza kuachiwa huru kwa Mbarushimana kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kumtia mbaroni kisheria.

Hata hivyo muda mfupi baadaye mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo Luis Moreno-Ocampo amesema kuwa ofisi yake itakata rufaa mara moja kupinga uamuzi huo wa majaji na kuagiza bwana Mbarushimana kuendelea kushikiliwa.

Mbarushimana ambaye anafahamika kama katibu mkuu wa kundi la waasi la nchini Rwanda FDLR anatuhumiwa kwa makosa 13 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu anayodaiwa kuyafanya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika jimbo la Kivu mnamo mwaka 2009.