KOREA KASKAZINI

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-il afariki dunia

Kiongozi wa taifa la Korea Kaskazini Kim Jong-il amefariki dunia siku ya Jumamosi wakati akiwa katika safari ya kuelekea katika vinu vya nyuklia vya Pyongyang, shirika la habari la nchi hiyo limeeleza. 

Matangazo ya kibiashara

Kim Jong-il ambaye alikuwa kiongozi wa taifa hilo toka mwaka 1994, ambapo alichukua madaraka hayo toka kwa baba yake na baadae kukiongoza chama chakikomunist ambacho ndicho kinaongoza nchi hiyo.

Kim ambaye anafariki akiwa na umri wa miaka 69 anaelezwa kuwa moja kati ya viongozi ambao wanaheshimika sana nchini mwake ambao inaelezwa toka achukue madaraka toka kwa baba yake amekuwa akilijenga jeshi la nchi hiyo kwa kiasi kikubwa.

Maelfu ya wananchi walionekana wakiangua kilio mara baada ya kutangazwa kwa kifo hicho huku wengi waliohojiwa walidai kuwa hawakutarajia kama kifo cha kiongozi huyo kingetokea ghafla namna hiyo.

Tayari chama cha Kikomunist nchini humo kilishamteua mtoto wa kiongozi huyo Kim Jong-Un kuwa mrithi wa baba yake ambapo taarifa zinasema kuwa yeye ndiye atakayesimamia mipango ya mazishi ya baba yake.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa uteuzi wa mtoto wa Kim Jong-il kushika madaraka ya kukiongoza chama cha kikomunist ni moja kati ya machaguo bora zaidi ambayo chama hicho imekifanya na kueleza kuwa atakuwa kiongozi mbadala atakayeendelea kutekeleza sera za baba yake.

Serikali ya korea Kaskazini imetangaza siku 12 kuwa za maombolezo kutokana na kifo hicho ambapo mazishi ya kiongozi huyo yamepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi huu.

Rais wa Korea Kusini Lee Myung-Bak ametoa wito kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kujipanga upya na kutazama jinsi gani watakavyoshughulikia suala la Korea Kaskazini huku ikielezwa kuwa tayari vikosi vya nchi hiyo vimepelekwa katika eneo la mpaka wa bahari kati ya nchi hizo mbili.