IRAN-UBELGIJI

Umoja wa Ulaya EU waiwekea nchi ya Iran vikwazo vya uuzaji wa mafuta

REUTERS/Francois Lenoir

Umoja wa Ulaya EU umekubaliana kuweka vikwazo vya mafuta dhidi ya nchi ya Iran sambamba na vile vya kifedha ikiwa ni muendelezo wa Mataifa ya Magharibi kuishinikiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa kurutubisha nyuklia na kuitaka kurejea kwenye meza ya pande sita ya mazungumzo.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umefikiwa kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya EU ulioketi Brussels nchini Ubelgiji na kufikia uamuzi wa kuongeza vikwazo kwa nchi hiyo iliyo njiani kutengeneza bomu la nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague amesema uamuzi huo ni muhimu sana hasa katika kuidhibiti nchi ya Iran kusonga mbele kwenye mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Waziri Hague amesema ni kitu sahihi kabisa kuweka vikwazo dhidi ya Tehran kwa kuwa nchi hiyo imekaidi Azimio la Barazala la Usalama la Umoja wa Mataifa UN juu ya mpango waker wa nyuklia.

Mkuu wa Masuala ya Mambo ya Nje kutoka Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton amesema shinikizo la kuiwekea vikwazo Tehran umekuja ili kusitisha mpango wa nchi hiyo kuendelea na kurutubisha madini ya uranium.

Ashton ameendelea kusema kuwa walitoa nafasi ya kutosha kwa Iran kuweza kurejea kwenye meza ya mazungumzo lakini wenyewe walionekana kukaidi uamuzi huo na njia ambayo ilikuwa imesalia ni kuweka vikwazo.

Nchi wanachama ishirini na saba wa Umoja wa Ulaya EU wameridhia vikwazo kwa nchi ya Iran kitu ambacho kinatajwa huenda kikaathiri uchumi wa taifa hilo na hivyo kusalimu amri kwenye mpango wake wa kurutubisha uranium.

Iran yenye imeendelea kuhubiri kila kukicha wanarutubisha madini ya uranium kwa sababu ya matumizi salama kwa wananchi wake ikiwemo ni pamoja na kutengeneza nishati ya umeme ya uhakika kwa taifa.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zilikuwa nchi za kwanza kutoka Umoja wa Ulaya EU kuafikiana kuiwekea vikwazo nchi ya Iran miezi mitatu iliyopita na kisha kuanza kampeni ya kushawishi mataifa mengine.