IRAN-UBELGIJI

Iran yasema vikwazo vya kuuza mafuta vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya EU si haki

Serikali ya Iran imesema hatua ya Umoja wa Ulaya EU kupitia Mawaziri wake wa Mambo ya Nje kuiwekea vikwazo vya kutonunua mafuta ya taifa hilo kutokana na yenyewe kuendeleza mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium si haki na hawatafaulu kwenye hilo.

Matangazo ya kibiashara

Tehran imesisitiza kuwa hatua hiyo ya kuwekewa vikwazo haitawarudisha nyuma kwenye mpango wao wa kuzalisha nyuklia ambayo kwa mujibu wa serikali ya Rais Mahmoud Ahmedinejad inatumika kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Ramin Mehmanparast amenukuliwa akisema kuwa urutubishaji wa madini ya uranium ambao unafanywa na nchi hiyo ni haki ya msingi kufanyika.

Mehmanparast ameongeza kuwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya EU umefikiwa kutokana na uwepo wa shinikizo kutoka kwa Marekani lakini ni amesema kuwa lazima nchi hizo zijue mahitaji ya Iran kabla ya kufanya uamuzi wowote.

Iran imeweka bayana kuwa Marekani inafanya haya yote kwa kuwa inasiri nzito lakini kwa kuwa nchi hiyo inachimba mafuta yake yenyewe na hata uranium inarutubishwa na wataalam wao wataendelea kusonga mbele tu.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton baada ya kuwekwa vikwazo hivyo alinukuliwa akisema ukaidi wa Iran ndiyo ambao umechangia taifa hilo kuwekewa vikwazo hivyo vya kuuza mafuta.

Marekani kupitia Rais wake Barack Obama imefurahishwa na uamuzi ambao umefikiwa na Umoja wa Ulaya EU katika kuiweka vikwazo nchi ya Iran wakiamini hiyo ndiyo njia pekee ya kuidhibiti kutekeleza mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya EU vinamaana kuwa hakuna nchi yoyote mwanachama ambayo itanunua mafuta kutoka nchini Iran huku wakizuia mali zote za nchi hizo zilizopo kwenye Benku Kuu ya Ulaya.

Mataifa ya Ulaya yalikuwa yananunua asilimia ishirini ya mafuta yote ambayo yanazalishwa nchini Iran baadhi ya wachambuzi wanahisi huenda hali hiyo ikateteresha uchumi wa nchi hiyo.