ISRAEL-PALESTINA

Umoja wa Ulaya EU wataka mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yaendelee

Reuters / Francois Lenoir

Umoja wa Ulaya EU umetoa wito kwa mataifa ya Mamlaka ya Palestina na Israel kuendelea na juhudi za mazungumzo ya kutafuta amani katika eneo la Mashariki ya Kati licha ya Wapalestina kudai kipindi hicho kimekwisha.

Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya EU Catherine Ashton ndiye ambaye ametoa wito huo wakati huu akiwa ziarani kwenye eneo la Ukingo wa Gaza kwa nia ya kukutana na Viongozi wa pande zote.

Ashton amesema ni kitu muhimu sana kuendeleza mazungumzo hayo na kuhakikisha wanafikia mafanikio yatakayokuwa na tija kwa wananchi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakihasimiana kwa miaka mingi.

Mataifa hayo mawili yanatarajiwa kuletwa pamoja kwenye mpango wa upatanishi unaondaliwa na nchi ya Jordan kwa lengo la kusafisha njia kabla ya kuanza kwa mazungumzo kamili ya kusaka amani ya kudumu.

Wananchi wa Palestina wanaamini muda ambao ulipangwa na wapatanishi wa kimataifa kuwasilisha mapendekezo yao unafikia kikomo kesho ingawa Israel inataka mazungumzo yaendelee.

Mgogoro baina ya Palestina na Israel umedumu kwa muda wakigombea mpaka kwenye eneo la Ukanda wa Gaza na Palestina ikipinga ujezi wa makazi mapya ya wayahudi unaofanywa na Israel.