Somalia-Uingereza

Hatma ya Somalia yajadiliwa nchini uingereza

Mkutano wa kimatsifa kuhusu Somalia, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na waziri mkuu wa Somalia Abdiweli mohamed
Mkutano wa kimatsifa kuhusu Somalia, waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na waziri mkuu wa Somalia Abdiweli mohamed

Viongozi kutoka mataifa hamsini duniani wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon wametaka hatua za haraka zichukuliwe kumaliza machafuko na hali ngumu ya kibinadamu ambayo inawakabili wananchi wa Somalia.

Matangazo ya kibiashara

Mkutano wa kujadili mustakabali wa Somalia uliitishwa Jijini London nchini Uingereza ambapo tishio la usalama kutokana na uwepo wa Kundi la Wanamgambo wa Al Shabab, uwepo wa ukame na vitendo vya uharamia ndiyo masuala makuu yaliyojadiliwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon alikuwa miongoni mwa wale ambao walipata bahati ya kuzungumza naye bila kificho chochote akasema kuna dalili za kupatikana kwa amani ya kudumu kitu ambacho hakistahili kuachwa.

Mkutano huu umefanyika nchini Uingereza chini ya uenyeji wake Waziri Mkuu David Cameron ambaye yeye akatumia fursa hiyo kuainisha matatizo ambayo wanakumbana nayo wananchi wa Somalia kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Marekani nayo ilihudhuria Mkutano huo wa kujadili hatima ya Somalia ambapo Mwakilishi wake alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton ambaye anaona njia pekee ya kukabiliana na Al Shabab ni kwa kusitisha vyanzo vyake vya mapato.

Abdiweli Mohammed Ali ni Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya Somalia inayoongozwa na Rais Sheikh Sharrif Ahmed ambaye anakiri utayari wa nchi yake kuruhusu kufanyika kwa operesheni za kijeshi kuwadhibiti Al Qaeda.

Kundi la Al Shabab limejibu kile ambacho kimejadiliwa na Mkutano huo kwa kusema kuwa wataendelea kukabiliana na Juhudi zozote za Kimataifa ambazo zitaazisha harakati za kurejesha amani katika nchi hiyo iliyo kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha zaidi ya miongo miwili.