MALAWI

Joyce Banda aapishwa kuwa rais wa nchi ya Malawi.

afrikeo.com

Aliyekuwa makamu wa rais wa Malawi Joyce Banda amewaambia wafuasi wake kuwa hakuna nafasi ya kulipiza kisasi baada ya yeye kuapishwa kuwa rais wa nchi hiyo na mwanamke wa pili barani Afrika kuongoza nchi,kufuatia kifo cha rais Bingu wa Mutharika siku mbili zilizopita.

Matangazo ya kibiashara

Banda alitoa maneno ya upatanisho kufuatia siku mbili za fitina za kisiasa ambapo duru za ndani za rais Mutharika zilijaribu kuzuia asipate nafasi hiyo ambayo ilikuwa inamwelekea yeye akiwa makamu wa rais kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Makofi ya pongezi na nyimbo za furaha zilisikika mara baada ya Banda kukamilisha kiapo cha urais na kisha kuwataka wananchi kukaa kimya kwa muda mfupi kwa ajili ya kumkumbuka rais Bingu ambaye yeye alimwita baba wa taifa.

Mutharika, akiwa na miaka 78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alhamis, ingawa kifo chake hakikuthibitishwa hadi Jumamosi jambo ambalo lilisababisha wasiwasi kuhusu nani anaongoza nchi hiyo.