OSLO-NORWAY

Breivik kuanza kujitetea hii leo kwenye mahakama kuu mjini Oslo

Anders Breivik mtuhumiwa wa mauaji nchini Norway akilia wakati akiangalia picha za video zilizomuonesha akitekeleza mauaji yake
Anders Breivik mtuhumiwa wa mauaji nchini Norway akilia wakati akiangalia picha za video zilizomuonesha akitekeleza mauaji yake Reuters

Mtuhumiwa wa mauaji ya watu sabini na saba kwenye mashambulizi mawili tofauti nchini Norway ambaye anatajwa ni Mtu mwenye msimamo mkali Anders Behring Breivik anatarajiwa kutoa ushahidi wake mwenyewe hii leo mbele ya Mahakama ya Oslo. 

Matangazo ya kibiashara

Breivik ambaye anatuhumiwa kutekeleza vifo hivyo mwezi Julai mwaka jana anatarajiwa kutoa ushahidi huo unaoelezwa na Mwanasheria wake Geir Lippestad kuwa utakuwa ni mgumu sana kuweza kuvumilika wakati ukisikilizwa pindi utakapokuwa unatolewa.

Breivik ambaye kwa mara ya kwanza alifikishwa Mahakamani huko Oslo jana alisema yeye hana hatia ya kutekeleza mauaji ambayo anahusishwa nayo na amekiri atajitetea kwa kueleza ukweli wote kwenye utetezi wake ambao utaanza kusikilizwa baadaye hii leo.

Breivik anatarajiwa kutoa utetezi wake wa kutekeleza shambulio alilolifanya kwa siku tano mfululizo mpaka pale atakapo maliza kabla ya upande wa mashtaka kuendelea kwa hatua zaidi ambapo nao pia ikibidi watawasilisha mashahidi wao.

Tayari mtuhumiwa huyo amewasili mahakamani hapo leo asubuhi na kuanza kutoa utetezi wake ambao umevuta hisia za watu wengi wakiwemo ndugu na jamaa wa waliopoteza maisha kwenye tukio hilo la mwezi Julai mwaka jana.

Hapo jana wakati wa ufunguzi wa kesi hiyo, mwendesha mashtaka wa serikali alionesha picha za video zilizokuwa zikimuonesha Breivik akitekeleza mauaji hayo, ambapo ilifikia wakati Breivik mwenyewe alitokwa na machozi baada ya kushindwa kuvumilia kile alichokuwa akikishuhudia.

Breivik mwenyewe amekana kuwa ni muuaji huku akikubali kutekeleza mauaji yake kwa kile anachodai kuwa alikuwa akijilinda dhidi ya maadui zake ambao anaeleza kuwa ni waislamu duniani kote.