SYRIA

Mapigano mapya yameripotiwa nchini Syria wakati huu ambapo waangalizi wa UN wako nchini humo

Wanajeshi wa Syria
Wanajeshi wa Syria Reuters

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ametaka Waangalizi wao ambao wamekwenda nchini Syria kujionea hatua ambazo zimepigwa katika kumaliza umwagaji wa damu wanapatiwa ulinzi wa uhakika wakati huu kukiwa na madai ya kuendelea kwa mashambulizi. 

Matangazo ya kibiashara

Ban amesema ni lazima serikali ihakikishe waangalizi hao sita wanakuwa kwenye mikono salama wakati wote hatua ambao imejibiwa na serikali ya Damascus watafanya hivyo iwapo watashirikishwa kikamilifu kwenye ziara hiyo.

Katibu Mkuu wa UN Ban amesema ni lazima pande zote zihusike kwenye ziara hii kitu ambacho kitasaidia pakubwa kuhakikisha makubaliano ya kisiasa yanafikiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Waangalizi hao Kanali Ahmad Himmiche amesema hadi sasa wamekuwa na mafanikio makubwa kwenye operesheni yao.

Serikali ya Rais Bashar Al Assad yenyewe imeendelea kusisitiza imeweka silaha chini lakini wapinzani ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kufanya mashambulizi.

Katika hatua nyingine kumeripotiwa mapigano mapya nchini humo kwenye baadhi ya miji kati ya vikosi vya serikali na vile vya majeshi huru ya Syria ambayo yanaipinga serikali ya rais Assad.

Serikali ya Syria imeutuhumu upinzani nchini humo kwa kuendelea mapigano wakati huu ambapo majeshi yake yameanza kuondoka kwenye miji ambayo ilikuwa inaikalia kama ilivyokubaliwa kwenye maazimio sita ya msuluhishi mkuu wa mgogoro huo, Koffi Annan.