MALI - GUINEA BISAU - ECOWAS

ECOWAS kuvituma vikosi vyake nchini Mali na Guinea Bisau

Wananchi wa Cote d'Ivoire wakiandamana jijini Abidjan wakati wa mkutano wa ECOWAS April 26
Wananchi wa Cote d'Ivoire wakiandamana jijini Abidjan wakati wa mkutano wa ECOWAS April 26 REUTERS/Luc Gnago

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS katika kikao chao jijini Abidjan nchini Cote d'Ivoire, wametowa taarifa ya kutuma vikosi vya kikanda nchini Mali na Guinea Bisau ili kulinda kipindi cha mpito katika nchi hizo mbili zinazo yumba kutokana na mzozo wa kisiasa na kijeshi. nchini Mali wanajeshi hao watatakiwa kulinda taasi za serikali ya mpito kabla ya mchakato wa kuandaa uchaguzi kufikia kikomo. Duru za karibu zaidi zaarifu kuwa vikosi hivyo vitazuia pia waasi wa kaskazini mwa Mali kuendelea kuteka miji mingine. kipindi cha mpito nchini humo kinataraji kufikia tamati katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Matangazo ya kibiashara

Kikao hicho cha nne cha ECOWAS kimepanga muda wa kipindi cha mpito nchini Mali cha mwaka mmoja, wakati katiba ya nchi hiyo inampa rais wa muda siku 40 kuandaa uchaguzi mkuu wa rais.

viongozi hao wa ECOWAS wamewataka wanajeshi walioendesha mapinduzi nchimi Mali Machi 22 kuheshimu makubaliano na katiba na kuwa chini ya uongozi wa utawala wa mpito unaoongozwa na serikali ya kiraia.

kuhusu waasi wa kaskazini wanaokalia thuluthi mbili za nchi hiyo, viongozi wa ECOWAS wameendelea kulaani waasi hao kuendelea kukalia miji ya Kidal, Gao, na Timbuktu, huku wakikiri na kuweka wazi msimamo wao wa kuheshimu mipaka ya nchi hiyo.

Viongozi hao wameomba pia yaanzishwe mazungumzo mara moja baina ya viongozi wa kipindi cha mpito na waasi wa kaskazini chini ya msuluhishi Blaise Compaore rais wa Burkinafaso ambae sasa atasaidiwa na rais wa Nigeria Goodluck Jonathan

Ama kuhusu kikosi cha ECOWAS kitacho undwa na wanajeshi 3000, hakuna muda maalum uliopangwa wa kuvutuma huko Mali. Lengo hasa itakuwa ni kulinda viongozi wa kipindi cha mpito nchini Mali na si kupambana na waasi wa kaskazini. Duru kutoka Abidjan zaarifu kuwa wanajeshi hao watakuwa pia na jukumu la kuzuia waasi wa kaskazini kusonga mbele kwenye uwanja wa mapambano kuelekea kusini.

Viongozi wa kundi la MNLA wamesema kuwa hawana lengo la kuendelea hadi kusini mwa nchi hiyo.