SYRIA

Vifo zaidi vyaendelea kutokea Nchini Syria kutokana na mapambano baina ya Jeshi la Serikali na Waasi

Mashambulizi ambayo yanaendelea kushuhudiwa nchini Syria katika Mji wa Idlib na kuleta madhara
Mashambulizi ambayo yanaendelea kushuhudiwa nchini Syria katika Mji wa Idlib na kuleta madhara Reuters / Sana

Watu ishirini na wanne wamepoteza maisha baada ya kuzuka kwa mapigano baina ya Wanajeshi watiifu kwa Rais Bashar Al Assad na Waasi ambapo raia kumi na wanajeshi kumi na mbili ni miongoni mwa watu waliopoteza maisha.

Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hili linakuja wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa UN ukitoa mwito mwingine kwa pande zinazohasimiana nchini Syria kuhakikisha wanaheshimu mapendekeo ya kumaliza machafuko ynayoendelea kushika kasi nchini humo.

Raia hao kumi wapoteza maisha kwenye shambulizi la bomu lililotokea katika Jiji la Idlib eneo ambalo linatambulika kama ngome imara ya Wapinzani nchini Syria wakati huu ambapo hali ya wasiwasi ikiendelea kutanda.

Miongoni mwa waliopoteza maisha kwenye shambulizi hilo la bomu ni pamoja na watu tisa kutoka familia moja ambao nyumba yao ilishambuliwa na mabomu yaliyorudha na Jeshi la Serikali ya Syria.

Wanaharakati nchini Syria wameendelea kutoa lawama zao kwa serikali ya nchi hiyo kutokana na kuendelea kufanya mashambulizi dhidi ya Wapinzani ambao wapo mstari wa mbele kutaka mabadiliko ya utawala.

Tukio hili linakuja baada ya hapo jana shambulizi la kujitoa mhanga kutekelezwa katika Jiji la Damascus ambapo serikali ya Rais Bashar Al Assad ililita ni la kigaidi na kusema hii ni ishara kwa wapinzani kutokata maridhiano.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon amezitaka pande zinazokinzana kufikia makubaliano na hatimaye kutekeleza mapendekezo ya Mpatanishi wa Kimataifa kwenye mgogoro huo Kofi Annan.

Ban amesema kinyume na hapo umwagaji wa damu ambao unaendelea nchini Syria hauwezi kuwa na kikomo kwani kila upande utaendelea kujipanga na kutekeleza mashambulizi dhidi ya wenzao na kuchangia vifo zaidi.

Mashambulizi haya yanaendelea kutokea licha ya uwepo wa Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN katika Miji ya Hama, Homs na Deraa ambao lengo lao ni kuhakikisha wanafanya tathmini ya utekelezwaji wa mapendekezo ya Annan.