UHISPANIA-UGIRIKI-UFARANSA-URENO

Wafanyakazi waadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani huku wakiendelea kushinikiza mazingira bora ya kazi

Wafanyakazi wakisherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa kufanya maandamano huku wakishinikiza mazingira bora ya kazi
Wafanyakazi wakisherehekea Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa kufanya maandamano huku wakishinikiza mazingira bora ya kazi

Wafanyakazi Duniani kote wameadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani huku maandamano makubwa yakishuhudiwa katika nchi nyingi za Ulaya kutokana na kuendelea kushinikiza nchi zao kuhakikisha zinaondoa mpango wao wa kubana matumizi kwa kupunguza wafanyakazi na kutaka huduma muhimu ziwafikie.Wafanyakazi katika nchi za Ulaya ikiwemo Ugiriki, Ureno na Uhispania wameandamana huku wakiwa na ghadhabu wakizilaumu serikali zao kwa hatua ya kubana matumizi ambazo wamezipendekeza ikiwa ni pamoja na kuwapunguza wafanyakazi ili kukuza uchumi wa nchi zao.

Matangazo ya kibiashara

Nchini Urusi Viongozi nao wameungana na wafanyakazi kwenye maandamano wakitaka serikali ya Moscow kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha wanaimarisha uchumi pamoja na kuwapa maslahi bora zaidi.

Siku ya Wafanyakazi Duniani imeonekana kukosa mashiko nchini Ufaransa kutokana na wananchi wa Taifa hilo kuwepo kwenye kampeni za duru la pili la uchaguzi wa rais ambao unatarajiwa kufanyika siku ya jumapili baina ya Rais Nicolas Sarkozy na Francois Hollande.

Wafanyakazi katika nchi za Asia nao wamesherehekea siku hii ya leo kwa kuendelea kudai mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi ambao wanadai bado serikali imeshindwa kuweka mazingira yanayostahili kwao ili wafanyekazi kwa uhuru.

Barani Afrika Wafanyakazi katika nchi nyingi wamesherehekea siku hi ya leo kwa kufanya maandamano pamoja na kuendelea kushinikiza nyongeza ya mishahara pamoja na kutaka kupunguziwa kodi.

Wafanyakazi wamezitaka serikali zao kuhakikisha wanatekeleza mapendekezo yao ili waweze kuendelea kutendakazi zao kwa ustadi na kuwaondolewa vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwakabili kwa muda mrefu sana.

Madai makubwa ya wafanyakazi dunia yameendelea kuwa ni ukosefu wa ajira za kudumu, usalama wao kazi pamoja na mazingira yasiyoridhisha ambayo wanakabiliana nayo mahali pa kazi.