INDIA

Zoezi la Uokoaji wa Manusura waliozama kwenye kivuko nchini India linaendelea kushika kasi

Wapigambizi wakiendelea kuopoa maiti za abiria waliopoteza maisha kwenye ajali ya kivuko nchini India
Wapigambizi wakiendelea kuopoa maiti za abiria waliopoteza maisha kwenye ajali ya kivuko nchini India

Wapigambizi na Kikosi Maalum cha Waokoaji nchini India wameendelea na zoezi la kusaka manusura wa ajali ya kivuko kilichozama katika Mto Brahmaputra uliopo kwenye Jimbo la Assam na kusababisha vifo vya watu mia moja na tatu hadi sasa.

Matangazo ya kibiashara

Zoezi hili la uokoaji linaendelea wakati huu ambapo Jeshi la Polisi likisema watu mia moja na hamsini wameokolewa licha ya watu wengine mia moja ambao walikuwa abiria kwenye kivuko hicho hawajulikani walipo.

Mkuu wa Jimbo la Assam Tarun Gogoi amesema idadi ya vifo huenda ikazidi kutokana na abiria wengi kutojulikana walipo licha ya zoezi la kuwasaka manusura kufanyika tangu usiku wa maneno lakini wanaonekana kugonga mwamba.

Ajali hiyo ya Kivuko imetokea umbali wa kilometa mia tatu na hamsini Magharibi mwa Jimbo la Assam kutoka Mji Mkuu wake Guwahati ambapo taarifa zinasema kuwa Kivuko hicho kilikatika pande mbili.

Kivuko hicho kinaelezwa kilikuwa na watu zaidi ya mia mbili pamoja na mizigo kitu ambacho kinaongeza hofu huenda wingi wa abiria na mizigo ndiyo umechangia kuzama kwa kivuko hicho.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema mkondo mkali wa maji ndiyo ambao umesababaisha vifo vya abiria wengi zaidi kutokana na wengi kusukumwa na maji ya mto Brahmaputra ambayo yanakasi kubwa zaidi.

Ajali za Vivuko nchini India zimekuwa ni za kawaida lakini ajali hii inatajwa kuwa ni mbaya zaidi kuwahi kutokea katika nchi hiyo ukilinganisha na ajali nyingine ambazo zimetokea katika miaka ya 2010 mwezi Juni na hata Oktoba.

Chanzo kikubwa cha ajali nchini India kimetajwa kuwa ni uchakavu wa vivuko pamoja na ukosefu wa usalama wa kutosha kwa vyombo hivyo ambavyo vingi vinamilikiwa na watu binafsi.