CHINA-MAREKANI

Mwanaharakati wa China Guangcheng aondoka Ubalozi wa Marekani baada ya kupata hifadhi kwa siku sita

Wanaharakati Chen Guangcheng mwenye ulemavu wa macho ametoka katika Ubalozi wa Marekani baada ya kupata hifadhi kwa siku sita
Wanaharakati Chen Guangcheng mwenye ulemavu wa macho ametoka katika Ubalozi wa Marekani baada ya kupata hifadhi kwa siku sita 路透社

Mwanaharakati wa China mwenye ulemavu wa macho ambaye alitoroka kifungo cha ndani na kisha kupatiwa hifadhi ya malazi katika Ubalozi wa Marekani Jiji Beijing Chen Guangcheng ameondoka Ubalozini kwa ajili ya kupatiwa matibabu sambamba na kuungana na familia yake Ofisa wa Marekani amethibitisha. Uamuzi wa kumuachia Guangcheng umekuja wakati huu ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton akizuru katika Taifa hilo ambapo serikali ya nchi hiyo imesema haitoendelea kuwakandamiza wanaharakati ambao wamekuwa wakikosoa utendaji kazi wao.

Matangazo ya kibiashara

Ofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini China amethibitisha kuachiwa kwa Mwanaharakati huyo wa Haki za Binadamu kuendelea na kuungana na familia yake kitendo ambacho kimepokelewa kwa mikono miwili na Guangcheng mwenyewe.

Serikali ya Beijing imeeleza utayari wake wa kutaka Guangcheng aende kuishi eneo salama katika nchi ya China baada ya kuomba hifadhi kwa siku sita ndani ya Ubalozi wa Marekani baada ya kukimbia kifungo cha ndani alichohukumiwa.

Guangcheng alionekana mksoaji mkubwa kwa serikali ambayo ilikuwa inashinikiza watu watoe mimba ikiwa ni sera mpya ya nchi hiyo inayotaka watu wasizae zaidi ya mtoto mmoja ili kuzuia ongezeko la watu.

Ofisa wa Ubalozi wa Marekani huko Beijing kwa mara ya kwanza ametoa ufafanuzi wa tukio hilo akisema walilazimika kumruhusu Guangcheng kuondfoka baada ya kuonekana makubaliano yamefikiwa baina ya pande zote mbili.

Saa kadhaa baada ya kuachiwa Mwanaharakati Guangcheng alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Clinton anatamani ambusu kutokana na kufanikisha mpango wa yeye kuwa huru baada ya kuishi kama mkimbi kwa siku sita.

Serikali ya China imesema itatoa ruhusa kwa maofisa wa Ubalozi wa Marekani pamoja na ndugu na jamaa zake kwenda kuonana na Guangcheng ambaye anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Beijing.

China imekuwa ikikosolewa sana kutokana na kubana uhuru wa Wanaharakati ambao wamekuwa wakikosoa sera mbalimbali za serikali kwani wakiamini zinawazuia kufanya shughuli zao ipasavyo.