AFGHANISTAN-MAREKANI

Rais wa Marekani Obama atangaza mwisho wa vita yao nchini Afghanistan ikiwa ni Mwaka mmoja baada ya Kifo cha Osama Bin Laden

Rais wa Marekani Barack Obama akisaini makubaliano na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai juu ya ahadi ambazo zitatekelezwa baada ya kumalizika kwa vita
Rais wa Marekani Barack Obama akisaini makubaliano na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai juu ya ahadi ambazo zitatekelezwa baada ya kumalizika kwa vita REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza rasmi mwisho wa vita yao nchini Afghanistan baada ya kufanikiwa kutekeleza hatua kama hiyo nchini Iraq kauli ambayo ameitoa alipofanya ziara ya kushtukiza huko Kabul kuangalia shughuli ambazo zinafanywa na majeshi ya nchi yake. Kinara huyo wa Dunia hakusita kusema kwa sasa mwanga unaanza kuonekana na ujio wa tumaini jipya unakaribia katika nchi ya Afghanistan huku akiamini wakati umefika kwa majeshi yake kumaliza vita hivyo kama ambavyo imefanya nchini Iraq na kuwaacha wananchi wa Afghanistan wajiendesha wenyewe.

Matangazo ya kibiashara

Ziara hiyo ya Rais Obama imekuja wakati huu ambapo umetimia mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden kwenye operesheni ya makomando wa Marekani ambayo ilifanyika nchini Pakistani alikokuwa anaishi.

Obama amesema lengo la nchi yake na majeshi yao ni kuhakikisha wanauangamiza Mtandao wa Al Qaeda na kwa sasa wapo kwenye sehemu nzuri ya kuhakikisha wanafanikiwa kutekeleza kile ambacho wamekuwa wamekipanga kwa muda mrefu.

Rais Obama amezungumza na wananchi wa Marekani katika Kambi ya Kijeshi ya Bagram ikiwa ni muda mchache baada ya kusaini makubaliano na Rais wa Afghanistan Hamid Karzai kuangalia ahadi ambazo zimetolewa na matarajio baada ya kumalizika kwa vita nchini humo.

Obama amesema hatua ambayo imefikia nchini Afghanistan inaonesha kila dalili za kmalizwa kwa vita hiyo na kuwarejesha nyumbani wanajeshi ambao walikuwepo katika Jeshi la Kulinda Amani nchini Afghanistan ISAF.

Rais Obama ameongeza kukamilika kwa vita ya Iraq kunawapa nafasi ya kufanya hivyo hivyo nchini Afghanistan na hatimaye kuacha jukumu la ulinzi wa amani kwenye mikono ya Jeshi la Serikali ya Kabul.

Wakati ziara hiyo inakamilika mlipuko mkubwa ulisikika nchini Afghanistan ambapo Wanamgambo wa Kundi la Taliban lilifanya mashambulizi kwenye kambi za kijeshi za kigeni kabla ya kuzimwa.