SYRIA

Wanajeshi 20 wauawa na Wapiganaji wa Waasi nchini Syria baada ya kuzuka kwa mapigano

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN waliopo nchini Syria kufanya tathmini wakiongozi na Mkuu wao Kanali Ahmed Himmiche
Waangalizi wa Umoja wa Mataifa UN waliopo nchini Syria kufanya tathmini wakiongozi na Mkuu wao Kanali Ahmed Himmiche Reuters/路透社

Jeshi la Syria kwa mara ya kwanza limepata pigo kubwa baada ya wanajeshi wake ishirini kuuawa na Wapiganaji wa Waasi tukio linlojiri majuma matatu baada ya Serikali ya Rais Bashar Al Assad kutangaza kusitisha mapigano ili kutekeleza mpango wa Mpatanishi wa Kimataifa Kofi Annan.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji wa Waasi wamewaua wanajeshi kumi na watano wa serikali ya Syria wakiwemo Wanajeshi wenye Vyeo vya Ukanali wawili baada ya kufanyika kwa shambulizi la kushtukiza katika Jimbo la Aleppo ambapo wapiganaji wawili walipoteza maisha.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu nchini Syria limethibitisha kutokea kwa shambulizi hilo na kuchangia vifo tukio lililotokea wakati Majeshi ya nchi hiyo yakiwa kwenye operesheni zake za kawaida.

Shambulizi jingine lilitokea karibu na Jiji la Damascus ambapo wanajeshi sita walipoteza maisha baada ya Jeshi nchini humo kuchoma nyumba za Wanaharakati Mashariki mwa Jimbo la Deir Ezzor.

Umwagaji wa damu huo unakuja siku moja baada ya Umoja wa Mataifa UN kupitia katibu Mkuu wake Ban Ki Moon kuzituhumu pande zote kutokana na kushindwa kutekeleza pendekezo la kumaliza mapigano.

Vifo hivi ni vya kwanza kuwalenga wanajeshi wa serikali ya Rais Assad tangu watangaze hatua ya kusitisha mapigano dhidi ya wapinzani tarehe 12 April mwaka huu kutekeleza mapendekezo ya Mpatanishi wa mgogoro wa nchi hiyo Kofi Annan.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa UN Herve Ladsous amesema Wanajeshi wa Serikali wameendelea kumiliki silaha nzito katika miji mbalimbali na kusema serikali na wapinzani wameshindwa kuheshimu makubaliano ya kusitisha mauaji.

Kauli ya Ladsous amesema hadi sasa Wanachama wa Umoja wa Mataifa UN wameidhinisha waangalizi 150 tu kuelekea nchini Syria badala ya 300 ambao walikuwa wanahitajika kufanya tathmini ya kutekelezwa kwa mapendekezo ya Annan.

Machafuko nchini Syria yamedumu kwa miezi 14 ambapo takwimu za Umoja wa Mataifa UN zinaonesha watu zaidi ya elfu tisa wapoteza maisha katika kipindi hiki chote kutokana na wapinzani kutaka mabadiliko ya utawala.