UFARANSA

Sarkozy na Hollande wapambana kwenye mdahalo wa Televisheni usiku kadhaa kabla ya Duru la Pili la Uchaguzi

Wagombea wa Duru la Pili la Uchaguzi nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Francois Hollande wakiwa kwenye mdahalo wa Televisheni
Wagombea wa Duru la Pili la Uchaguzi nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Francois Hollande wakiwa kwenye mdahalo wa Televisheni

Wagombea na Urais nchini Ufaransa kwenye duru la pili ambao ni Rais anayetetea wadhifa wake Nicolas Sarkozy na Mpinzani wake ambaye aliibuka mshindi kwenye duru la kwanza kutoka Chama Cha Kisoshalisiti Francois Hollande wamepambana vikali kwenye mdahalo wa Televisheni kabla ya uchaguzi wa jumapili.

Matangazo ya kibiashara

Wagombea hao kila mmoja ametumia vyema fursa hiyo kujinadi kwa wananchi wa Ufaransa ambao wanatarajia kutumia haki yao ya kupiga kura siku ya jumapili kuamua nani awe rais kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika ya Sarkozy na Hollande ambao walipata kura nyingi kwenye duru la kwanza.

Mdahalo huo uliodumu kwa saa mbili na dakika hamsini ulitoa nafasi nzuri kwa wananchi wa Ufaransa kuendelea kupima sera za wagombea hao ambao kila mmoja amekuwa akikosoa sera za mwingine na hata ilifika kipindi walianza kurushiana maneno makali.

Kabla ya kufanyika kwa mdahalo huu ambao ulikuwa unaliliwa zaidi ya Rais Sarkozy mpinzani wake Hollande alikuwa anapingana na wazo hilo lakini Rais anayetetea wadhifa wake akaendelea kusisitiza hii ndiyo hatua sahihi ya kuweka bayana ukweli wa mambo kwa sasa.

Hollande kwenye mdahalo huo aliendelea kujikita kwenye sera zake za kiuchumi na kuahidi kuinua uchumi wa wananchi wa taifa hilo pamoja na kusema ataongoza kwa uwazi na kujiepusha yeye kuwa mtu wa mwisho wa kufanya maamuzi na badala yake atashusha madaraka chini.

Rais Sarkozy akijibu sera hiyo ya uchumi amejigamba kwamba amekuwa akifanya vizuri kwa kipindi chake cha miaka mitano na ndiyo maana nchi ya Ufaransa haijatetereka kiuchumi ukilinganisha na mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya EU.

Hollande akashindulia msumari mwigine kwa kumtuhumu Rais Sarkozy kwa kushindwa kulinda heshima yake kwenye jamii na hivyo akajiapiza yeye kuhakikisha anakuwa na tabia njema ambayo itawapendeza hata wananchi.

Wagombea hao kila mmoja kwa wakati wake alishuhudiwa akimuita mwenzake muongo wakati mdahalo unaendelea kushika kasi kutokana na takwimu au maelezo ambayo anayatoa dhidi ya mwezie.

Kura za maoni hadi sasa zinaonesha Hollande ana nafasi kubwa ya kushinda duru la pili kwa asilimia kati ya 53 hadi 54 dhidi ya Sarkozy ambaye anaendelea kuhaha kuhakikisha anatetea wadhifa wake.