SYRIA

Wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu Cha Aleppo nchini Syria wauawa kwenye shambulizi la Jeshi

Waandamanaji nchini Syria wanaopinga utawala wakiwa wamechora ukuta wa Chuo Kikuu Cha Aleppo kilichofungwa baada ya kutokea vifo vya wanafunzi wanne
Waandamanaji nchini Syria wanaopinga utawala wakiwa wamechora ukuta wa Chuo Kikuu Cha Aleppo kilichofungwa baada ya kutokea vifo vya wanafunzi wanne

Uongozi wa Chuo Kikuu Cha Aleppo kilichopo nchini Syria kilichoshambuliwa na wanajeshi na kusababisha vifo vya wanafunzi wanne na kukamatwa wengine 200 umetangaza kukifunga Chuo hucho hadi tarehe 13 May.

Matangazo ya kibiashara

Chuo hicho kilichopo Kaskazini mwa nchi ya Syria kimefungwa hadi tarehe 13 May ambapo mitihani itaanza rasmi taarifa ya Uongozi wa Chuo hicho imetumwa kwenye mtandao kutoa taarifa kwa wanafunzi.

Wanaharakati nchini Syria wamethibitisha kufungwa kwa Chuo Cha Aleppo pamoja na kuzuiliwa kwa wanafunzi kuingia kwenye eneo hilo kwani hata mabweni ya wanafunzi yameshafungwa.

Jeshi la Syria chini ya Rais Bashar Al Assad lilishambulia Chuo Kikuu Cha Aleppo baada ya wanafunzi wake kufanya maandamano kuungana na wapinzani wakishinikiza mabadiliko ya utawala katika nchi hiyo.

Mtandao wa Chuo Kikuu umesema mashambulizi baina ya wanafunzi na Jeshi la nchi hiyo yamechangia kuleta hofu katika eneo hilo ndiyo sababu ambayo imechangia kusitishwa kwa masomo kwa sasa ili kurejesha usalama.

Mapambano ambayo yametokea katika Chuo Kikuu Cha Aleppo yanatajwa kuleta uharibifu mkubwa wa eneo la Chuo pamoja na majengo ambayo yanatumika kama madarasa pamoja na mabweni ya wanafunzi.

Wanaharakati nchini Syria wamesema Jeshi liliamua kufanya mashambulizi hayo kuzima maandamano ya kupinga utawala ambayo yamezidi kushika kasi katika nchi hiyo tangu kuanza kwake miezi 14 iliyopita.