UFARANSA

Kampeni za Duru la Pili la Uchaguzi wa Urais nchini Ufaransa kumalizika huku Hollande akiongoza kura za maoni

Wagombea wa Duru la Pili la Uchaguzi nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Francois Hollande kabla ya kufanyika kwa uchaguzi siku ya jumapili
Wagombea wa Duru la Pili la Uchaguzi nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Francois Hollande kabla ya kufanyika kwa uchaguzi siku ya jumapili Reuters

Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Kisoshalisti nchini Ufaransa Francois Hollande yupo kwenye nafasi nzuri ya kushinda duru la pili la uchaguzi baada ya kura za moani zilizofanyika baada ya mdahalo baina yake na Rais Nicolas Sarkozy kuonesha anasilimia kubwa za kupata ushindi. Kura za maoni ambazo zimefanyika siku moja baada ya Mdahalo ulioendeshwa kwa njia ya Televisheni kati ya Hollande na Sarkozy umemuongezea nafasi kubwa ya ushindi mgombea huyo kutoka Chama Cha Kisoshalisti.

Matangazo ya kibiashara

Akiungwa mkono na Mshindi wa nne wa Duru la kwanza la Uchaguzi Francois Bayrou mgombea kutoka Chama Cha Kisoshalisti Hollande amejikusanyia asilimi 53 ya kura zote huku mpinzani wake kwenye kinyang'anyiro cha pili Sarkozy akiambulia asilimia 47 pekee.

Kampeni za Uchaguzi duru la pili zinakamilika hii leo ambapo wagombea wote wawili wanapiga kampeni za mwisho kuomba ridhaa kutoka kwa wananchi wa Ufaransa ili aweze kuongoza nchi hiyo kwa miaka mitano.

Hollande mshindi wa duru la kwanza la uchaguzi amesema kama wananchi wa Ufaransa wanataka kuchagua ni lazima wahakikishe wanafanya hivyo kwa kuchagua mtu sahihi wa kuongoza nchi hiyo katika kipindi hiki.

Sarkozy kwa upande wake amesema ana imani atafanikiwa kuibuka mshindi kwenye duru la pili dhidi ya mpinzani wake Hollande baada ya kuanguka kwenye kinyang'anyiro cha duru la kwanza.

Mdahalo kupitia Televisheni ambao ulifanyika siku ya jumatano ulitoa nafasi kwa wananchi wa Ufaransa kuona namna ambavyo wagombea hao wawili wanavyopanga hoja zao na sera walizonazo.

Mpambano baina ya wagombea hao wawili umejiegemeza kwenye sera za kiuchumi ambapo Hollande amekuwa akikosoa sera za Sarkozy ambaye anajigamba kufanikiwa kuimarisha uchumi wa Taifa hilo.