CHINA-MAREKANI

Mwanaharakati wa China Guangcheng aendelea kusaka msaada wa Marekani ili aweze kuodoka nchini mwake na familia yake

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Nchini China mwenye ulemavu wa macho Chen Guangchen ameendelea kupeleka kilio chake kwa serikali ya Marekani kuisihi impatie hifadhi kwani anaona maisha yake yapo hatari pamoja na familia yake huku akiona kama ametelekezwa kwa sasa.

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu nchini China Chen Guangcheng akiwa na Ofisa wa Marekani Kurt Campbell
Mwanaharakati wa Haki za Binadamu nchini China Chen Guangcheng akiwa na Ofisa wa Marekani Kurt Campbell REUTERS/US Embassy Beijing Press Office/Handout
Matangazo ya kibiashara

Guangchen ameendelea kushinikiza kupatiwa hifadhi na hivyo kuelekea kuishi uhamishoni pale ambapo amezungumza na Kamati ya Bunge ya Marekani inayoshughulikia masuala ya China kwa njia ya simu ambapo amesema usalama wake na familia yake umezidi kuwa hatari.

Mwanaharakati huyo ambaye anaendelea kupata matibabu katika Hospital ya Beijing amesema iwapo itashindikana kupatiwa hifadhi nchini Marekani basi maisha yake yatazidi kuwa hatarini zaidi kutokana na kuendelea kuikosoa serikali.

Guangcheng ameiambia Kamati ya Bunge ya Marekani kuwa ameshindwa kuwa na utulivu katika kipindi cha miaka kumi kutokana na kusakamwa na serikali ya Beijing ambayo imekuwa mstari wa mbele kukandamiza haki za binadamu.

Mwanaharakati huyo bila ya kung'ata maneno amesema hajui hatima na usalama wa mama yake pamoja na kaka zake ambao wanaandamwa na serikali kutokana na kazi ambazo amekuwa akizifanya yeye.

Guangcheng amesema matumaini yake ataelekea nchini Marekani kwa kutumia ndege aliyosafiria Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye yupo China kwenye ziara ya kiserikali.

Mwanaharakati huyo ambaye alipatiwa hifadhi kwa siku sita katika Ubalozi wa Marekani baada ya kukimbia kifungo cha nyumbani amekuwa akipinga sera ya serikali inayohalalisha utoaji wa mimba ili kukabiliana na ongezeko la watu.

Katika hatua nyingine Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema Mwanaharakati Guangcheng anayo nafasi ya kwenda kusoma ughaibuni kwani haki hiyo ni ya kila mwananchi wa Taifa hilo.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje Liu Weimin katika taarifa yake ameeleza kuwa Guangcheng ana uhuru wa kuomba na kisha kwenda kusoma katika chuo chochote nje ya nchi.