MAREKANI-PAKISTAN

Nyaraka za siri za Osama Bin Laden zachapishwa na kuonesha hofu aliyokuwa nayo kabla ya kifo chake

Serikali ya Marekani imetoa nyaraka za siri zilizokuwa zinamilikiwa na Kiongozi wa Mtandao wa Kigaidi Duniani Marehemu Osama Bin Laden zikionesha wasiwasi aliokuwa nao Kiongozi huyo kuhusu mtandao wake na shughuli ambazo walikuwa wanazifanya.

Kiongozi wa zamani wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden kabla ya kifo chake
Kiongozi wa zamani wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden kabla ya kifo chake @Reuters
Matangazo ya kibiashara

Nyaraka hizo zimeonesha bayana hofu ambayo alikuwa nayo Osama kabla ya kifo chake juu ya idadi kubwa ya vifo ambayo vinavyowakabili raia wanaoishi katika nchi za Kiislam pamoja na wafuasi wake waliopo nchini Pakistan.

Kwenye nyaraka hizo kunaonesha namna ambavyo Osama alishikwa na hofu kutokana na kupoteza au kukosa ushirikiano wa kutoka kutoka kwa Makundi mengine duniani likiwemo Al Shabab linalopatikana nchini Somalia.

Barua 17 za Osama ndizo ambazo zimechapishwa na kubeba ujumbe huo mzito ambao ulionesha namna ambavyo hofu ya kuanguka kwa Al Qaeda kutokana na baadhi ya majaribio yao kushindwa.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo Osama amesema alitaka kundi lake kuendelea kushambulia Ofisi zote za Marekani Duniani isipokuwa katika nchi za Iraq na Afghanistan akihofia kutokea kwa vifo vya wananchi wasio na hatia.

Osama anahisi kama mashambulizi yake yangefanyika nchini Iraq na Afghanistan ni wazi kabisa mashambulizi hayo yangechochea vifo vya raia wa mataifa hayo ambao hawahusiki kwenye tukio hilo.

Hofu nyingine ambayo alikuwa nayo Osama ni kuuawa kwa baadhi ya Viongozi wa Al Qaeda katika nchi za Pakistan kitu ambacho alikuwa anahisi kilikuwa kinadhohofisha nguvu ambayo waliyokuwa nayo.

Nyaraka hizi zinatolewa ikiwa ni mwaka mmoja tangu kutekelezwa kwa kifo cha Osama Bin Laden kilichofanikishwa na Makomando wa Marekani waliofanya operesheni maalum nchini Pakistan.