IRAQ

Polisi wa Interpol watoa waranti ya kukamatwa kwa makamu wa rais wa Iraq, Tareq Al Hashemi

Makamu wa rais wa Iraq Tariq al-Hashemi ambaye ametolewa hati ya kukamatwa Polisi wa Interpol
Makamu wa rais wa Iraq Tariq al-Hashemi ambaye ametolewa hati ya kukamatwa Polisi wa Interpol Reuters

Polisi wa Kimataifa wanaofahamika vizuri kwa jina la Interpol wametoa waranti ya kukamatwa kwa Makamu wa Rais wa Iraq Tareq Al Hashemi ambaye anatuhumiwa kufanya mauaji pamoja na kufadhili mashambulizi ya kigaidi. 

Matangazo ya kibiashara

Waranti hiyo imegusa nchi zote za ukanda huo pamoja na mataifa ya mengine wanachama mia moja na tisini wa Interpol wakisema ni lazima akamatwe ili akumbane na mkono wa sheria kujibu mashtaka ambayo yanamkabili.

Interpol imesema waranti yao imekuja baada ya serikali ya Iraq kuanzisha uchunguzi dhidi ya Al Hashemi kutokana na makosa ya mauaji na kufadhili mashambulizi ya kigaidi ambayo yametendeka nchini mwake.

Al Hashemi ambaye inasemekana anapatiwa hifadhi nchini Uturuki hakuwepo Mahakamani wakati kesi yake iliposikilizwa kwa mara ya kwanza ambapo yeye na walinzi wake wanatuhumiwa kuwaua majaji sita pamoja na maofisa waandamizi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona kuwa kukamatwa kwa kiongozi huyo kutachangia kuongezeka kwa machafuko nchini Iraq kwakuwa makamu huyo wa rais anawafuasi wengi ambao wanamuunga mkono.

Kinachosubiriwa sasa ni kauli ya Serikali ya Uturuki kuhusu kumkamata ama kutomkamata kiongozi huyo ambaye amedai kuwa hatotendewa haki iwapo kesi yake itasikilizwa nchini Iraq.